Uongozi wa Simba umesema umepania kumpa zawadi JPM kupitia michuano hiyo ya Afrika ambayo kwa sasa ipo hatua ya makundi na wao wakiwa kinara wa kundi A wakiwazidi ujanja vigogo Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na Al Merrikh ya Sudan kwa kufika hadi nusu fainali ama fainali yenyewe msimu huu.
Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kuna msukumo mkubwa walikuwa wanaupata kutoka kwa JPM enzi za uhai wake kila alipokutana na viongozi wa klabu hiyo na hasa alipokuwa akisikia wamefanya kitu kizuri.
Try Again alisema JPM kila alipokuwa akisikia Simba imefanya vizuri alikuwa akiwataka kuanzia hapo kujipanga vizuri zaidi ili wafanye mambo makubwa katika michuano ya Afrika kwa kutanguliza umakini na kuacha ubabaishaji.
“Ilikuwa kila akisikia tumeshinda anayekutana naye na kumpa salamu hizo huwa aanamuachia ujumbe akisema kawaambie wamefanya vizuri, ila nataka kuona wanafanikiwa zaidi huko Afrika,” alisema Try Again mmoja kati wa wajumbe wenye nguvu ya maamuzi ndani ya klabu hiyo.
“Mnakumbuka aliwahi kutusema tulipofungwa na Kagera Sugar? Ile kwetu ilikuwa kama njia ya kutufanya tujipange zaidi na hakuishia hapo aliendelea kututumia salamu za kututaka tuweke pembeni maandalizi ya zimamoto na tujenge timu ya kweli.”
Bosi huyo alisema kupitia salamu hizo za JPM waliweka nia ya kujipanga vizuri zaidi katika michuano ya Afrika na sasa wanaona faida ya salamu zake kwao.
“Sasa tunafanya vizuri ndani na hata Afrika, ninachoweza kusema haya ni matunda ya kutuhimiza kwake, tulikaa kama bodi na kusema tuweke nguvu ya kutosha ili tufikie malengo ambayo mkuu wa nchi anayataka,” alisema Try Again.
Aidha Abdallah alisema katika kumuenzi JPM Simba inataka kuhakikisha inafika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika au hata fainali ili iwe ni zawadi kwa kiongozi huyo shupavu aliyekuwa mdau mkubwa wa klabu hiyo ya Msimbazi.
“Tunataka kufanya kitu kwa kumuenzi mchango wake unajua miaka sita hii hakuna klabu ambayo inaweza kupita mbele yetu na kusema imefanikiwa kushinda Simba, tupo katika hatua kubwa ya kufika robo fainali,” alisema Tray Again na kuongeza;
“Ila bodi yetu na klabu kwa ujumla hatutaki kuishia hapo tunataka kufika nusu fainali au ikiwezekana fainali kabisa,tukifika hapo tutaona ni zawadi kubwa kwetu kwa Rais wetu huyu mpendwa ambaye kiukweli amelifanyia makubwa taifa hili.”
Ili wafike huko ni lazima Simba ihakikishe inawanyoosha Waarabu ambao wamekuwa wakitawala kwenye hatua hizo za juu ya michuano hiyo ya Afrika, kwani mpaka sasa zilizotangulia robo fainali ni Wydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Simba, imeshatanguliza mguu mmoja robo fainali ikiongoza kundi A ikiwa na pointi 10 ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama 7, kisha AS Vita iliyokusanya pointi nne na Al Merrikh inaburuza mkia na alama moja tu.