MTAMBO wa mabao ndani ya kikosi cha Azam FC, Prince Dube amebakiza dakika 270 za kukutana na mshikaji wake wa Yanga, Bakari Mwamnyeto ambaye ni beki.
Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, George Lwandamina mkononi ina mechi 10 za kuhitimisha ligi, itakutana na wapinzani wao Yanga baada ya kucheza mechi tatu ambazo ni dakika 270.
Itaanza na Mtibwa Sugar, Aprili 9, itakuwa na kazi mbele ya JKT Tanzania, Aprili 16 kisha itakutana na Dodoma Jiji, Aprili 22 baada ya mechi hizo Dube atakutana na mshikaji wake Mwamnyeto kwenye mchezo wa ligi utakaochezwa Aprili 25, Uwanja wa Mkapa.
Raia huyo wa Zimbabwe anakumbukumbu ya kupata maumivu ya mkono walipokutana na Mwamnyeto kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex na kumfanya akae nje kwa muda wa wiki sita akipewa matibabu.
Mchezo huo ulikamilika kwa ubao kusoma Azam FC 0-1 Yanga na bao lilipachikwa na Deus Kaseke hivyo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa sababu Azam itahitaji kulipa kisasi na Yanga nao wanahitaji kulinda rekodi.