SELEMAN Matola, kocha msaidizi wa Klabu ya Simba amesema kuwa wanatambua wapinzani wao Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika watawakamia ili kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Mkapa ila wanaamini hawataweza.
Leo Simba ina kazi ya kusaka ushindi mbele ya Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki Uwanja wa taifa wa Cairo. Msafara wa Simba una jumla ya watu 55 ambapo wachezaji ni 26 viongozi na benchi la ufundi 29.
Akizungumza na Saleh Jembe, Matola amesema kuwa wanawatambua wapinzani wao na wanawaheshimu kwa kuwa ni timu bora ili haitaweza kupata ushindi kirahisi.
“Walikuja Uwanja wa Mkapa tukawafunga sasa tunawafuata na tunajua hesabu zao ni kuona kwamba wanashinda mchezo huo hawataweza kwani tupo imara na wachezaji wamepewa majukumu ya kufanya.
“Yupo nahodha John Bocco, kurejea kwake kunaleta matumaini, wachezaji wote wanacheza kwa kushirikiana hali ambayo inatupa nguvu ya kupata matokeo ugenini, tunahitaji kulinda rekodi ya kutofungwa katika hatua ya makundi,” amesema Matola.
Timu zote mbili kwenye kundi A zimetinga hatua ya makundi ampabo Simba ina pointi 13 na Al Ahly ina pointi 8.