LICHA ya Tottenham kuanza kupachika bao la kuongoza dakika ya 40 ngoma ilikuwa ngumu kwao kusepa na pointi tatu muhimu baada ya wapinzani wao Manchester United kupindua meza kibabe.
Baada ya dakika 90 kukamilika ubao wa Uwanja wa Tottenham Hotspur ulisoma, Tottenham 1-3 Manchester United.
Ni Son Heung-min alianza kutikisa nyavu dakika ya 40 na kuwafanya United kwenda mapumziko wakiwa hawajaona lango la wapinzani wao.
Kipindi cha pili United ilipachika bao la kuweka mzani sawa dakika ya 57 kupitia kwa Fred, Edinson Cavan akaongeza msumari wa pili dakika ya 79 na Mason Greenwood alipachika msumari wa mwisho dakika ya 90+6.
Ushindi huo unaifanya Manchester United kufikisha pointi 63 ikiwa nafasi ya pili na Tottenham inabaki na pointi 49 nafasi ya 7 zote zimecheza mechi 31 ndani ya Ligi Kuu England.
Kinara ni Manchester City mwenye pointi 74 baada ya kucheza mechi 32 huku mabingwa watetezi Liverpool wakiwa nafasi ya 6 na pointi 52 na wamecheza mechi 31.