IMEELEZWA kuwa mabosi wa Yanga wameamua kuwaengua mastaa wa kikosi hicho ambao hawana mchango mkubwa katika kikosi hicho ili kufanya usajili mpya.
Habari kutoka chanzo cha kuaminika zimeeleza kuwa tayari baadhi ya wachezaji wameanza kupewa taarifa kwamba hawataongezewa mikataba pale ambapo msimu utakwisha.
Kwa sasa Yanga ipo nafasi ya kwanza na pointi 51 kwenye msimamo ikiwa imecheza jumla ya mechi 24 huku watani zao wa jadi Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi 49 wamecheza mechi 21.
Mtoa taarifa huyo amesema:”Kuna wachezaji ambao wameambiwa kwamba hawataongezewa mikataba pale muda wao ukiisha miongoni mwao ni pamoja na Fiston Abdulazack ambaye hajawa kwenye ubora wake.
“Pia Michael Sarpong huyu naye kuna hatihati akaachwa kwa kuwa nafasi yake imezidi kuwa ndogo kikosi cha kwanza na hafungi mabao kama ilivyo kazi yake, yule Muangola, (Carlos Carlinhos) amebadilika hivyo akiendelea kuwa hivyo atakutana na adhabu pia.
“Orodha ni ndefu na panga ambalo litapita ni kubwa ukitazama Wazir Junior, Farid Mussa hawa kubaki itakuwa ngumu, Ditram Nchimbi huyu bado wanamtazama kwa kuwa amekuwa na mchango kiasi chake licha ya wengi kumlalamikia kwamba hafungi.
“Lengo la kufanya hivi ni kuboresha kikosi na juzi mabosi walikutana kujadili namna ya kufanya maboresho ya kikosi cha Yanga,” ilieleza taarifa hiyo.
Hivi karibuni, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa alisema kuwa wanatarajia kuwaacha baadhi ya wachezaji ambao wanaonekana kutokidhi mahitaji.