MTATHIMINI viwango wa timu ya Simba,Culvin Mavhunga amefunguka kuwa kwa sasa akili yake ipo kwenye mechi za kimataifa kuona ni timu gani ambayo itapangwa kucheza na Simba kwenye hatua ya Robo Fainali ili aweze kuingia chimbo na kusaka mafaili yao.
Simba imekuwa kwenye kiwango bora katika michuano ya kimataifa huku nyuma ya pazia kazi kubwa ikifanywa na Mzimbabwe huyu ambaye alijiunga na Simba, Januari na tangu amejiunga na timu hiyo imekuwa kwenye kiwango bora.
Akizungumza na Championi Ijumaa, juzi Jumatano kwenye mchezo ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya
Mtibwa Sugar, Mavhunga alisema: “Kwa sasa tuna michezo kadhaa ya ligi ambayo ninaamini tutazidi kufanyia vizuri, lakini kwa sasa nimejikita zaidi kuwasoma wapinzani wetu ambao tunatarajia kukutana nao kwenye hatua ya Robo Fainali ya Caf kuona tutaingia na staili gani.
“Jambo la kufurahisha ni kuwa tutaanzia ugenini, hivyo nina imani itakuwa rahisi kwetu kwenye mchezo wa marudio ambao tutakuwa nyumbani, kazi yangu kubwa ni kuhakikisha naandaa taarifa ambayo inakwenda kumrahisishia kazi mwalimu.”
Simba inatarajia kukutana na MC Alger, CR Belouizdad au Kaizer Chiefs kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo droo ya Robo Fainali inatarajiwa kupangwa Aprili 30,2021.