THOBIAS Kifaru, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar amesema kuwa kwa sasa timu hiyo inahitaji maombi kutoka kwa wadau pamoja na mashabiki ili itimize lengo la kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22.
Ikiwa imecheza jumla ya mechi 24 ambazo ni dakika 2,160 imekusanya pointi 24 ina wastani wa kukusanya pointi moja kila baada ya dakika 90 ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo.
Kifaru amesema kuwa hawapo kwenye nafasi nzuri kwa wakati huu kutokana na matokeo yasiyoridhisha licha ya kuwa na kikosi bora.
“Tumekutana na kimbunga kwa sasa ambacho ni cha ajabu kwetu, tunahitaji maombi kutoka kwa wadau pamoja na mashabiki ili tuweze kutimiza malengo yetu ya kubaki ndani ya ligi hii ambayo tuna historia nayo nzuri.
“Unajua ukisema kwa sasa Mtibwa Sugar ishuke sasa hapo nani ambaye ataleta ushindani kwa timu nyingine ambazo zinafanya vizuri? Pale ambapo tumekosea benchi la ufundi linafanyia kazi kisha tukiweza kupata ushindi kwenye mechi zetu tuna imani kwamba tutabaki,” amesema.
Baada ya kupoteza kwa kufungwa mabao 5-0 dhidi ya Simba Uwanja wa Mkapa, leo ina kibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya Kagera Sugar, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.