RASMI European Super League Cup imesimamishwa baada ya timu zote ambazo zilikubali kushiriki ligi hiyo mpya kujitoa jumlajumla kutokana na shinikizo kutoka kwa mashabiki kupinga ligi hiyo pamoja na Uefa kuigomea kabisa.
Mashabiki wengi walikuwa wanaigomea ligi hiyo mpya ambayo ilikuwa inahusisha timu zenye uwezo mkubwa kifedha na tayari timu 15 zilikuwa zimekubali kushiriki ligi hiyo iliyokuwa inapingana na Uefa pamoja na Fifa.
Miongoni mwa mashabiki ambao walijitokeza kupinga ligi hiyo ni pamoja na wale wa Chelsea ambao kabla ya mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Stamford Bridge dhidi ya Brighton na kukamilika kwa sare ya bila kufungana walikuwa wakiishinikiza timu hiyo ijitoe kwa kuwa ilikuwa ni miongoni mwa timu ambazo zilikubali kushiriki ligi hiyo mpya.
Timu kubwa ambazo zilikubali kushiriki ligi hiyo ambayo ilianza fukuto Aprili 18,2021 na kuzimwa Aprili 20, ikiwa ni pamoja na Manchester United, Liverpool, Arsenal, Real Madrid, Barcelona, Atletico Madrid na Tottenham nazo pia zilithibitisha kujitoa kwenye ligi hiyo ambayo Shirikisho la Soka la Ulaya, Uefa liliweka wazi kuwa wote ambao watashiriki michuano hiyo mipya watafungiwa haraka sana.