PRINCE Dube kinara wa utupiaji ndani ya kikosi cha Azam FC kesho anatarajiwa kuongoza jeshi la timu hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji.
Nyota huyo mwenye mabao 10 na pasi sita za mabao alikosekana kwenye mchezo wa ligi dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Dube alikosekana kwenye mchezo huo kutokana na kuwa na kadi tatu za njano jambo ambalo lilimfanya akosekana kwenye mchezo huo.
Mbali na Dube, pia nyota wao Brunce Kangwa ambaye ni beki naye pia alikosekana kwenye mchezo huo kutokana na kuwa na kadi tatu za njano hivyo naye adhabu yake imemeguka.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa adhabu ya nyota hao imekwisha hivyo wana nafasi za kuanza kwenye mchezo wa kesho.
“Ile adhabu ya kadi tatu za njano walizokuwa wakitumikia, Prince Dube na Kangwa, (Bruce) tayari imekwisha hivyo ana nafasi ya kuanza kesho mbele ya Dodoma Jiji,” .
Azam FC kwenye msimamo ipo nafasi ya tatu na ina pointi 50 baada ya kucheza jumla ya mechi 26 inakutana na Dodoma Jiji iliyo nafasi ya 6 na ina pointi 37.
Baada ya kumalizana na Dodoma Jiji, Azam FC ina kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Yanga, Uwanja wa Mkapa, Aprili 25 hivyo ikiwa watakuwa kwenye ubora nyota hao wana nafasi ya kuwawahi wapinzani hao pia.