ULIMWENGU wa michezo unashuhudia wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa ambao wanaendelea kufanya vizuri kwenye kila mechi ambazo wanacheza na kuyapata mafanikio makubwa ambayo kila mmoja anahitaji kuona yakitokea.
Katika hayo yote ambayo yanaendelea ukifuatilia kwa umakini utagundua kwamba wachezaji hao hawapo kwenye mkumbo wa makosa mengi ya kuwa na jeuri pamoja na kiburi bali wanaishi katika misingi na ile ya kanuni kwa kuishi kwenye nidhamu.
Ipo wazi ukiachana na suala la michezo hata kwenye suala la mafaniko katika hali ya kawaida pamoja na uchumi bado nguzo yake kubwa imejengwa kwenye nidhamu ikiwa ni pamoja na matumizi ya muda pamoja na kile ambacho unakipata.
Hili ni somo ambalo wachezaji wengi wakubwa wamekuwa wakianguka ghafla pale ambapo wanapata mafanikio na kusahau kwamba maisha huwa yanabadilika ila kanuni zinaishi na hazibadiliki zaidi ya kuboresha ili kuwa bora zaidi.
Wapo wachezaji wengi wazuri hapa Bongo ila wamekwama kupata timu nje ya nchi kwa sababu ya suala la nidhamu. Wapo pia wachezaji wengine ambao wameachwa na timu zao kutokana na suala la nidhamu na hawatazami uwezo katika hili.
Hapa kuna kitu cha kujifunza kwa sababu hivi karibuni kumekuwa na matukio kwa wachezaji kufanya vituko licha ya kwamba kuwa na uwezo mkubwa katika kutimiza majukumu yao.
Achana na Ligi Kuu Bara mpaka Ligi Daraja la Kwanza na lile la Pili kumekuwa na matukio ambayo hayafurahishi na maisha yao yanaendelea kama ambavyo wanafikiria ila hawatambui kwamba anguko kwao linakuja.
Kesi za wachezaji kuamua kucheza chini kiwango kisa kumkomoa mwalimu ama kugoma kukaa benchi wakihitaji kuanza kikosi cha kwanza zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara wakati huu.
Hii ni mbaya kwa wachezaji kuonyesha matendo ambayo hayaleti afya kwenye soka letu la Tanzania ambalo linazidi kupenya anga kwa kukua kwa kasi.
Inasikitisha pale ambapo mchezaji wa kigeni anafanya mambo ya ovyo uwanjani ilihali anatambua kwamba kuna namna ya kuweza kuzuia suala hilo na maisha yakaendelea.
Ipo wazi kwamba kukoseana kupo kwa timu zote lakini pale ambapo hisia zinakuwa tofauti na mmoja kati ya mchezaji kuamua kuzionesha hisia hizo nje hilo ni baya na halipaswi kupewa nafasi.
Jambo la msingi kwa wachezaji wote Tanzania wanapaswa waheshimu yale ambayo wanaambiwa wayafanye na hata kama ikitokea wataanzia benchi basi wanajukumu la kulinda nidhamu.
Mwalimu anajua aina ya wachezaji ambao anahitaji kuanza nao kwenye kikosi ili kupata ushidni wale ambao wanakasirika inaonesha kwamba wanampangia majukumu mwalimu.
Wapo wachezaji ambao imeripotiwa kwamba wamekuwa wakigombana kwenye timu zao bila sababu hii ni mbaya na haipaswi kupewa nafasi lazima nidhamu ifuate mkondo wake.
Miongoni mwa wachezaji wenye majina na bado wanaishi kwenye nidhamu yao ni pamoja na Lionel Messi wa Barcelona, Cristiano Ronaldo wapo wengi ambao wanaendelea kuwa mifano na wanafanikiwa kwa zama zao.
Pia wachezaji wanapaswa wajue kwamba timu ni kubwa kuliko mchezaji, mchezaji utacheza kwa wakati uliopo na utaondoka ila timu itabaki daima na milele.