MOJA ya timu ambayo imefanikiwa kupata mafanikio makubwa sana kwenye soka kwa muda mfupi ni KMC ya Kinondoni.
Timu hii ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kujipambanua na kuonyesha ni jinsi gani ni timu bora.Kuanzia wamepanda daraja mwaka 2017 imekuwa ni timu tishio sana kwenye Ligi Kuu Bara.
Unaweza kusema kuwa imepata kwenye mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi labda kuliko timu nyingi kwenye ligi hiyo kwa kuwa ndani ya misimu mitatu tu wameshapata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shrikisho Afrika.
Hata kama hawakufanya vizuri lakini nafikiri ni funzo kwao kuwa siku moja wanaweza kufanya vizuri kama wakifanya maandalizi mazuri ya michuano hiyo mikubwa Afrika.
Sare ya bao 1-1 na Yanga kwenye mzunguko wa pili huku wenyewe wakionekana kuutawala mchezaji kwa sehemu kubwa inaonyesha kuwa kama kuna timu inataka kuifunga KMC basi ni lazima ifanye maandalizi ya kutosha.
Lakini pia pamoja na safu yao ya ulinzi bado kuna picha inaonekana kwenye safu ya ulinzi ya KMC ambayo kwenye michezo 27 waliyocheza pia wamefungwa mabao 19 pia inashika nafasi ya nne kwenye timu zilizofungwa mabao machache msimu huu.
KMC wamezidiwa na Simba ambayo imefungwa mabao tisa, Yanga imefungwa mabao 16 na Azam mabao 19. KMC wanapambana na timu kubwa tatu za Dar es Salaam, inapambana kimafanikio na Azam, Simba na Yanga.
Lakini pia hata kimfumo wa uendeshaji KMC wanatakiwa kurekebisha mambo machache tu lakini kiuhalisia ni kwamba wanakwenda kwenye mafanikio makubwa sana ya soka kama watakubali kuwa wavumilivu na kutengeneza timu yao taratibu.
Mfano idara ya habari ya KMC ni moja ya idara ambayo inaonekana kuwa bora kwa sasa, ukitaka kufahamu jambo lolote kuhusu KMC unalipata haraka tena kwa wakati, nafikiri hili ni jambo ambalo hata Simba, Yanga na Azam wanatakiwa kujifunza huku.
Jambo lolote la KMC ambalo vyombo vya habari vinatakiwa kulifahamu limekuwa likisambaa haraka sana na kila mpenda michezo amekuwa akilipata, hapa nafikiri watakuwa na kazi ndogo ya kuboresha.
Lakini pia jambo pekee ambalo KMC wanatakiwa pia kulifanya ni kutojilinganisha na Simba, Yanga na Azam kwa sasa, wanatakiwa kuendelea kufanya mambo yao taratibu na kuziheshimu timu hizo kwa kuwa zimetangulia, lakini wakiamini kuwa muda utaongea.
Kuingia katikati ya Simba, Yanga na Azam haiwezi kuwa kazi rahisi kwao, lakini uvumilivu unaweza kuwafanya wakafika hapo haraka.