LEO muda wowote, kipa Metacha Mnata anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga Yanga.
Kipa huyo hivi karibuni aliingia kwenye mgogoro na timu hiyo mara baada ya kuandika ujumbe wa kuaga saa chache baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania uliomalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kipa huyo ndani ya wiki hii kuanzia leo Jumanne, huenda akapewa mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kukipiga Yanga, huku pia akirudishwa kikosi cha kwanza baada ya Farouk Shikalo kuonekana kuwa na makosa ya wazi.
Mtoa taarifa huyo alisema kipa huyo atasaini mkataba huo baada ya kufikia makubaliano mazuri kati ya kipa na uongozi wa timu hiyo Aliongeza kuwa, benchi la ufundi na uongozi wamembakisha kipa huyo baada ya kutomuona kipa mwingine mzawa mwenye uwezo wa kuichezea Yanga katika msimu ujao.
“Benchi la Ufundi la Yanga na uongozi kwa pamoja tumekubaliana kuwa hakuna haja ya kumuachia Metacha aondoke na tumchukue kipa mwingine wa kiwango cha juu kama alichokuwa nacho Metacha.
“Hivyo uongozi umefikia makubaliano mazuri na Metacha kwa ajili ya kumuongezea mkataba mpya wa kuendelea kuichezea Yanga katika misimu mingine miwili.
“Hiyo ni baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Lakini pia atarudi kikosi cha kwanza na Shikalo akipumzishwa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuzungumzia hilo hilo, simu yake ya mkononi iliita bila ya mafanikio ya kupokelewa.