KAMATI ya Katiba na Kamati ya Mabadiliko wamekamilisha ripoti ya muundo pendekezwa na kukabidhi kwa Kamati ya Utendaji ya Yanga.
Ripoti hiyo alikabidhiwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wa sekretarieti mara baada ya kukamilika.
Hiyo inaamanisha mfumo pendekezwa wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu ya Yanga kukamilika rasmi chini ya kamati iliyokuwa inaongozwa na mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa.
Msolla alisema kuwa mfumo huo pendekezwa wa mabadiliko ya uendeshaji wa Yanga umekamilika rasmi na hivi sasa wanakwenda katika hatua nyingine.
Msolla alisema kuwa kilichobakia hivi sasa ni kufuata muongozo na baraka kutoka kwa washika dau wa michezo ambao ni wizara yenye dhamana na michezo, Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Fair Competition Commission (FCC), TFF na Bodi ya Ligi Kuu Bara.
“Baada ya kukamilika vitu vyote hivyo, semina elekezi kwa viongozi wa matawi zitatolewa kwa madhumuni ya kusambaza elimu ya mabadiliko haya na pia kupokea maoni ya wanachama ili kuyafanya mabadiliko haya kuwa shirikishi na yenye maslahi mapana ya klabu yetu.
“Mwisho kabisa ni Mkutano Mkuu wa Wanachama utakaofanyika kupata uamuzi na baraka za wanachama kuelekea mabadiliko ambayo mashabiki wanayasubiria.
“Niahidi kukamilisha hilo jambo kwa haraka ili nifanikishe sehemu ya ahadi yangu niliyoitoa kipindi cha uchaguzi kwa kuahidi kukamilisha mfumo wa mabadiliko ambao hivi sasa upo mwishoni kukamilika,” alisema Msolla.
Chanzo:Championi