Home Azam FC AZAM FC BADO WAKOMALIA JAMBO LAO

AZAM FC BADO WAKOMALIA JAMBO LAO

 VIVIER Bahati Kocha Msaidizi wa Azam FC amesema kuwa bado jambo lao lipo palepale licha ya jana, Aprili 22, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ubao kusoma Dodoma Jiji 2-2 Azam FC.

Sare hiyo inakuwa ni ya 9 kwa msimu huu wa 2020/21 baada ya kucheza jumla ya mechi 27 huku jambo lao ikiwa ni kutwaa ubingwa wa ligi ulio mikononi mwa Simba. 

Ni Prince Dube alipachika bao la kuongoza dakika ya 2 lilidumu mpaka kipindi cha pili na kumfanya nyota huyo kufikisha jumla ya mabao 11 ndani ya ligi.

Dube anakuwa namba moja kwa utupiaji ndani ya Azam FC pamoja na kwenye ligi wakiwa sawa na nyota wa Simba, Meddie Kagere.

Kipindi cha pili mambo yalibadilika ambapo Seif Karihe aliweka usawa dakika ya 71 na likaongezwa la pili dakika ya 77 na Anuary Jabiry.

Shukran kwa Obrey Chirwa ambaye alipachika bao lake la kuipa pointi moja Azam FC dakika ya 90+5.

Kwenye msimamo wa ligi Azam FC ipo nafasi ya 3 na pointi zake ni 51 na Dodoma Jiji ipo nafasi ya 6 na pointi zake ni 38.

Bahati amesema:”Bado tunaendelea kupambana kwani malengo yetu ilikuwa kupata pointi tatu ila tumeshindwa kutokana na wapinzani wetu kupata mabao.

“Jambo letu lipo palepale tutaendelea kupambana kwa mechi ambazo zimebaki,”.

Mchezo unaofuata kwa Azam FC ni dhidi ya Yanga ambao unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Aprili 25 saa 2:15 usiku ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, ubao ulisoma Azam FC 0-1 Yanga.


SOMA NA HII  AZAM FC KAMILI KWA AJILI YA NAMUNGO FC