Home Simba SC MEDDIE KAGERE: MSIHOFU , MWARABU ANAFUNGIKA HATA KWAO,

MEDDIE KAGERE: MSIHOFU , MWARABU ANAFUNGIKA HATA KWAO,

 


USIKU wa leo Ijumaa, timu yetu ya Simba itakamilisha ratiba ya mechi za Kundi A kwa kucheza ugenini dhidi ya Al Ahly kabla ya kusubiri kujua itavaana na nani kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika – michuano mikubwa kabisa kwa ngazi za klabu barani Afrika.

Bahati nzuri tunacheza mechi ya mwisho tukiwa tumejihakikisha kumaliza kama vinara wa kundi A na pia kusonga mbele sambamba na wapinzani wetu wa leo, ikiwa tumefanikiwa kutimiza lengo tulilojiwekea kabla ya kuanza kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa msimu huu.

Nakumbuka miongoni mwa kolamu zangu zilizopita nilieleza faida za kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi letu, ikiwemo aina ya timu ambayo tunakwenda kukutana nayo pamoja na faida ya kuanzia mechi ya robo fainali ugenini na kumalizia nyumbani.

Baada ya kufanikiwa hili katika mechi hii ya ugenini na Al Ahly tunataka kumaliza na heshima ambayo tumeanza nayo hatua ya makundi kucheza mechi sita bila kupoteza mchezo wowote.

Kama kuna mtu anadhani kwa kumaliza vinara na kujihakikisha kucheza robo fainali kutafanya tubweteke na kukubali kupoteza mchezo ugenini, pole yake. Tumepania kulinda heshima yetu.

Tumecheza mechi tano ambazo zote hakuna tuliyopoteza – iwe nyumbani au ugenini, kwani tumeshinda ugenini dhidi ya AS Vita na kupata suluhu Sudan tulipocheza na Al Merrikh pia tumeshinda mechi zote tatu za nyumbani dhidi ya Al Ahly, Al Merrikh na AS Vita.

Kwa maana hiyo katika mechi hii ya Al Ahly licha ya kuonekana tunaenda huku tukiwa tumefuzu bado tunataka kulinda heshima ya kutopoteza mechi mpaka tunacheza nusu fainali.

Siyo kazi rahisi kucheza mechi ya ugenini dhidi ya Al Ahly wakiwa nyumbani ukamaliza dakika 90 bila kufungwa, lakini tutakwenda kupambana ili kufanikiwa kutofungwa kwa kuamini hata wao wanafungika kwao. Kama tuliweza kuwanyoosha AS Vita kwao hatuoni sababu ya kushindwa kufanya hivyo leo Cairo. Kila kitu kinawezekana.

Ukipata nafasi ya kuangalia mechi yetu utaona aina ya mbinu ambazo tunakwenda kucheza nazo ni zile ambazo tunahitaji kucheza mechi bila kupoteza kama ilivyokuwa mechi zetu mbili za awali.

Unajua litakuwa jambo la faida kwetu tunaenda kucheza mechi ya robo fainali huku tukiwa tumecheza mechi ya mwisho katika mashindano hayo dhidi ya timu kubwa na mabingwa watetezi nyumbani kwao, Al Ahly, bila kufungwa.

SOMA NA HII  PACHA YA MUGALU NA BOCCO YAMKOSHA KOCHA SIMBA

Unajua tunafahamu mashabiki wengi wana ari na morari kubwa wakiamini tunakwenda kucheza mechi hii huku tukiwa tumefuzu kwenye hatua ya robo fainali, tutaingia katika mchezo tukiwa na jambo hilo akilini.

Kwetu wachezaji, benchi la ufundi na msafara mzima tuliokuja huku Misri tumepanga kupambana kutafuta matokeo mazuri tofauti ya kutofungwa ingawa tunatambua utakuwa siyo mchezo rahisi kwani tunacheza na mabingwa watetezi wa kombe hili.

Al Ahly katika mechi ya mzunguko tuliwafunga mchezo wa nyumbani kwetu, sidhani kama watakubali kupoteza kwa mara ya pili wakiwa katika ardhi yao.

Al Ahly wanafahamu ubora wetu katika mashindano haya, lakini tupo nafasi ya kwanza dhidi yao, lazima watapambana kwelikweli ili kutaka kupata pointi kama ambavyo nasi hatutakubali kirahisi.

Mara ya mwisho tulipokuja kucheza mechi katika nchi hii tulipoteza kwa idadi kubwa ya mabao ambayo hatutamani kuona tunakutana nayo tena, kwani msimu huu tumeimarika zaidi ya wakati ule.

Tutakuwa na nidhamu ya kufanya vizuri dhidi yao au kutopoteza kwa idadi kubwa ya mabao kama ambavyo ilikuwa wakati ule kwani ilikuwa historia mbaya kwa upande wetu.

Hivyo, tunaingia kwenye mechi hii tukiwa na akili kubwa ya kufanya vizuri huku tukisahau historia ambayo tumeifanya au kuipata katika mashindano haya hasa katika hatua hii ya makundi.

Si hivyo tu, lakini pia tumepania kuhakikisha msimu huu tunamaliza kwa heshima kubwa kuliko msimu wa 2018-2019.

Katika msimu huo tulimaliza wa pili kundi nyuma ya Al Ahly na kisha kwenda kutolewa katika mechi za robo fainali na TP Mazembe ya DR Congo, lakini safari hii tukimalizana na Al Ahly. 

Tutajipanga ili kuhakikisha timu yoyote tutakayokutana nayo robo fainali tunawanyoosha nje ndani. Tunaamini hili linawezekana kwa rekodi tuliyoweka msimu huu kwa kumaliza vinara wa kundi na alama 13, mabao tisa ya kufunga na kufungwa moja, huku tukishinda mechi nne kati ya tano na kuwa mbele ya watetezi – Al Ahly – walio na pointi nane kwa sasa baada ya mechi tano.