Home Simba SC RALLY BWALYA – YANGA WALIZIDIWA NA SIMBA KWENYE KUNISAJILI KWA SABABU HII..!!

RALLY BWALYA – YANGA WALIZIDIWA NA SIMBA KWENYE KUNISAJILI KWA SABABU HII..!!


MIONGONI mwa nyota wa kigeni wanaocheza na kuonyesha viwango bora kwenye Ligi Kuu Bara ni kiungo wa Simba, Mzambia Rally Bwalya. Staa huyo alisajiliwa Simba kabla ya msimu huu kuanza kwa mkataba wa miaka miwili akitokea timu ya Power Dynamos iliyopo Ligi Kuu ya Zambia.

Katika mahojiano na gazeti la Mwanaspoti, kiungo huyo mwenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto anaelezea mambo mbalimbali na namna alivyotua Simba huku akiacha ofa nyingine ikiwemo ya Yanga.

Anasema baada ya Yanga kumfuata wakati huohuo Simba walikuwa wamefika, lakini katika kutafuta taarifa za kutosha ipi timu sahihi kuchezea kura nyingi ziliangukia Simba. “Ilibidi nikubaliane na Simba na kusaini mkataba, wakati huo Yanga walikuwa kwenye mchakato wa kunifuata Zambia ili kunisainisha,” anasema.

“Niliwaeleza ukweli Yanga kuwa kuna moja ya timu ambayo nimekubaliana nayo na nakwenda kusaini mkataba, lakini hawakutaka kuelewa na badala yake muda wananifuata Zambia nilikuwa njiani kuja Tanzania.

“Tulimepishana nao, wao wanafika Zambia mimi na Chriss Mugalu ndio tulikuwa tumefika Tanzania – tena tulikuwa ndege moja bila kujuana tulikuja kuonana uwanja wa ndege wakati tunapokelewa.”

CHAMA KUMVUTA

Miongoni mwa wachezaji ambao walihusika kumvuta Bwalya Simba ni kiungo Clatous Chama.

“Nilitenga muda kuwafuatilia Simba kutokana na taarifa ambazo nilizipata kutoka maeneo yangu mbalimbali, lakini nilizungumza na Chama ambaye alinihakikishia kuwa ni timu sahihi ambayo nafaa kucheza,” anasema.

“Chama nafahamiana naye siku nyingi, tumecheza mpira wote Zambia na tupo pamoja timu ya taifa, ikawa sina budi kumsikiliza ndipo nilikubali kutua Simba. Najivunia uamuzi huo kwani Simba ni miongoni mwa timu zenye malengo makubwa na inaweza kumuinua mchezaji.”

LIGI KUU BARA

kuhusu Ligi Kuu Bara, Bwalya anasema: “Ligi Kuu ya Tanzania inakua kwa kasi kila mwaka na ni yenye ushindani mkubwa bila ya kujali timu ndogo zinakutana au nyingine zimemzidi mwenzake.

“Kila ukiangalia mechi yoyote timu ambayo inapata ushindi lazima ipambane vya kutosha kwani kila moja inakuwa na lengo la kushinda ila ile ambayo inakuwa bora katika siku hiyo ndio inashinda.

“Ukiangalia licha ya ukubwa wa Simba na ubora wa kikosi chetu kilivyo, tumekutana na ugumu wa mechi kuna ambazo tumetoka sare na nyingine mbili tumepoteza tena katika uwanja wa nyumbani na ugenini.”

UBORA WAKE

Kuwepo kwa wachezaji wengi wenye viwango bora ndani ya Simba kumeisaidia kuimarisha kikosi hicho ambapo wengine hawapati nafasi ya kucheza ingawa nao wana viwango vizuri.

“Ili nicheze kwa mafanikio ndani ya Simba natakiwa kujituma zaidi ya ambavyo naonekana sasa kwani timu hii haihitaji mchezaji ambaye hana msaada,” anasema.

“Naamini nikiendelea kuwepo Simba kwa muda mrefu nitakuwa bora zaidi ya wakati huu ambavyo watu wanadhani, kwani najifahamu nikicheza eneo ambalo nimelizoea kwa muda mrefu kama ilivyokuwa Zambia nakuwaje.”

MECHI BORA

Bwalya anasema mechi kati yao na JKT Tanzania ilikuwa bab’kubwa.

“Mechi ya JKT Tanzania iliyochezwa Dodoma ndio ilikuwa mwanzo mzuri kwangu kufanya vizuri kwenye ligi kwani nilicheza soka la hali ya juu pamoja na kuisaidia timu yangu kushinda mabao 4-0.

SOMA NA HII  YANGA WAZIDI KUIGHARAGAZA SIMBA KILA KONA...MASUDI DJUMA AFUGUKA ISHU NZIMA ILIVYO..

“Nakumbuka mechi hiyo licha ya kucheza vizuri nilitoa pasi ya mwisho kwa Meddie Kagere ambaye naye aliitumia vizuri kwa kuifungia timu moja ya mabao kati ya yale manne.”

MASHABIKI WA SOKA

Bwalya anasema miongoni mwa mambo yanayochangia maendeleo ya soka ni uwepo wa mashabiki wanaotakiwa kuwa na msisimko wa matokeo na kile kinachoendelea.

“Ligi ya Tanzania imekuwa ikifuatiliwa maeneo mbalimbali na miongoni mwa sababu ambazo zinachangia ni mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani kushangilia timu zao,” anasema.

“Ligi ya Tanzania imeongezeka thamani miongoni mwa sababu ni mashabiki kupenda timu zao na soka kwa ujumla.”

KIKOSI CHA KWANZA

Chini ya kocha Sven Vandenbroeck, Bwalya alikuwa akiingia na kutoka kikosi cha kwanza na kuna wakati hakupata nafasi ya kucheza.

Tangu amefika Didier Gomes, Bwalya amekuwa mchezaji mwenye uhakika wa namba kikosi cha kwanza.

“Jambo ambalo limenisaidia mpaka kuingia kikosi cha kwanza kocha wetu mpya ni mkali na anapenda kusimamia zaidi nidhamu. Nimekuwa nikionyesha nidhamu pamoja na kujituma zaidi mazoezini ndiyo maana napata nafasi.

“Nikipata nafasi ya kucheza, napenda kufanya zaidi ya kile ambacho nimeonyesha mazoezini ili aendelee kunipatia nafasi mara nyingine, maana nakuwa ni mchezaji ambaye nimehusika kutoa mchango timu kufanya vizuri,” anasema.

MWISHO WA MSIMU

“Tumebakiwa na mechi nyingi mbele yetu, lakini naamini tunaweza kufanya vizuri na tukafikia malengo yetu kutwaa mataji yaliyo mbele,” anasema Bwalya.

“Simba ni timu inayohitaji mataji kila mashindano ambayo tunashiriki na malengo yapo hivyo, ndio maana ikitokea tumepata matokeo mabaya tunakuwa na wakati mgumu.

“Mwisho wa msimu naiona Simba itatetea ubingwa wa ligi pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC) na kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika.”

ANAYEMVUTIA

Bwalya anasema kuna wachezaji wengi wenye uwezo kulingana na nafasi ambazo wanazitumikia kwani wamekuwa bora katika kutimiza majukumu yao ila hawafanani kama vidole vya mkono vilivyo.

“Niseme tu ukweli navutiwa zaidi na Chama, anacheza soka lake, amekuwa msaada, amehusika katika matokeo mazuri lakini kuna mambo mengi najifunza kutoka kwake, amekuwa mbunifu kwa kusumbua wapinzani.”

SIMBA, YANGA

Bwalya anazungumziaje ushindani uliopo kati ya Sima na Yanga? “Ushindani huo unachangia kukua kwa ligi na nchi kufahamika, lakini unachangia wachezaji bora na wenye majina makubwa kutamani kuja kucheza katika timu hizi.

“Ushindani ni mkubwa na unaongeza msisimiko wa ligi na kila timu kushindana na kila timu ambazo inakutana nazo ili kufanya vizuri,” anasema.

MECHI YA YANGA

Bwalya anasema hakuwa anafahamu ukubwa wa kikosi cha Yanga pindi inapokutana na Simba, lakini siku chache kabla ya mchezo wake wa kwanza aligundua zilivyo na msimsimko katika soka nchini.

“Nilianza kuona ubishani katika mitandao ya kijamii na amshaamsha maeneo mengi wakizungumzia mechi hiyo kwani hata mazoezini mashabiki walikuwa wakija kwa wingi.

“Nimefurahi kucheza mechi hii kwani naamini kuna vitu nimejifunza na wakati mwingine ambao nitapata nafasi kama hiyo tena nitaonyesha kiwango bora zaidi,” anasema Bwalya.