Home Simba SC SIMBA vs AS VITA | GOMES – TUNAKUJA KIVINGINE

SIMBA vs AS VITA | GOMES – TUNAKUJA KIVINGINE


KAMA uliangalia mechi ya Simba ya ugenini dhidi ya AS Vita ukiwa na presha muda wote kutokana na staili ile ya kujilinda, basi raundi hii jiandae kushangilia tu katika mechi ijayo Jumamosi kwani kocha Didier Gomes amesema watakuja kivingine.

Katika mechi ile ya DR Congo, Simba ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Chris Mugalu kwa penalti akiwa kwenye ardhi ya nyumbani kwao, lakini mashabiki wa Msimbazi walijawa na hofu kutokana na muda mwingi timu yao kujilinda.

Nyota wao kama Luis Miquissone na Luis Chama ambao wanatisha kama umeme wanaposhambulia, siku ile walicheza chini sana na presha iliwapanda mapema mashabiki baada ya wachezaji wa Vita kukosa mabao kadhaa ya mapema ikiwamo kugongesha nguzo ya lango. Vita siku ile walikuwa hatari sana pia kwa mipira za adhabu zikiwamo kona, lakini mara hii kocha Gomes amesema: “Subirini muone watakavyopoteana.”

Gomes amesema jinsi ambavyo wataingia na kucheza ni tofauti na ilivyokuwa mchezo wa awali, ambapo sasa analenga zaidi ushindi na sio sare.

Alisema kuwa mechi ya mzunguko wa kwanza ugenini kule DR Congo walicheza kwa kuzuia zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza na hata bao walilopata lilitokana na matunda ya staili ile.

“Mechi hii itakuwa tofauti na tulivyocheza ugenini, tutawaheshimu wapinzani ambao watakuja kwa kutaka ushindi ili kutafuta nafasi ya kufuzu robo fainali. Utofauti ambao utakuwepo tutacheza kwa kushambulia zaidi ili kutafuta mabao na kumaliza mapema, hatutakubali kusubiri mpaka dakika za jioni kwa kukwepa kucheza kwa presha,” alisema Gomes.

Simba inayoongoza Kundi A ikiwa na alama 10, inahitaji pointi moja tu kufuzu robo fainali huku ikibakiwa na mechi moja ya ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri yenye alama 7.

AS VITA WABADILIKA

Katika hatua nyingine, Gomes alisema ametenga muda wa kutosha kufuatilia mechi za AS Vita kupitia kanda za video na kubaini wapinzani wao wamebadilika maeneo mengi tofauti na walivyocheza nao.

Gomes alisema mabadiliko hayo ya AS Vita ni mambo ya kiufundi ambayo akiyaweka hadharani atakuwa kama anauza silaha na huenda watajirekebisha na kucheza kivingine jambo ambalo litaongeza ugumu wa mechi.

SOMA NA HII  SAPRAIZI YA MWISHO SIMBA HII HAPA.....MASHINE YA KAZI KUTAMBULISHWA...YANGA WALIMTAKA...

“Mabadiliko hayo kuna mahali wamekuwa bora lakini kuna sehemu nyingine wana udhaifu. Kutokana na muda mchache uliobaki nitatenga darasa kwa wachezaji wangu na kuwaelekeza kupitia video za mechi mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa;

“Baada ya hapo tutafanya mazoezi ya vitendo uwanjani kutokana na vile ambavyo tumeviona ili kuona namna gani tutawazuia na kuwashambulia ili kupata mabao.”

SHUNGU PRESHA JUU

Kocha msaidizi wa AS Vita, Raoul Shungu alisema kikosi cha Simba msimu huu kimebadilika na kuwa bora zaidi ya msimu wa 2019, walipowafunga mabao 5-0, mechi ya nyumbani kwao.

“Simba msimu huu ni timu ambayo ukicheza nayo unatakiwa kuwa na tahadhari nayo. Simba wameimarika zaidi kutokana na baadhi ya wachezaji waliowaongeza. Hii itakuwa ngumu sana.”