Home Simba SC SIMBA SC ‘WAICHAKATA’ GWAMBINA FC NA KUKALIA USUKANI WA LIGI

SIMBA SC ‘WAICHAKATA’ GWAMBINA FC NA KUKALIA USUKANI WA LIGI

 


Bao pekee lililofungwa na Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Junior’ katika mchezo dhidi ya Gwambina FC, limetosha kuipandisha Simba SC kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom tukifikisha alama 58.

Zimbwe alifunga bao hilo kwa shuti kali la nje ya eneo la hatari lililomshinda golikipa wa Gwambina, Mohammed Makaka na kugonga  juu ya goli kabla ya kuingia wavuni moja kwa moja.

Katika mchezo wa leo Simba SC walicheza zaidi mipira mirefu ya juu kitu ambacho si kawaida yao kutokana na uwanja kuwa mbovu katika eneo la kuchezea.

Dakika ya 74 mlinzi Joash Onyango alifunga bao kwa  kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Clatous Chama lakini mwamuzi msaidizi namba moja alilikataa kwa kusema mpira ulitoka kabla kufungwa.

Kocha Didier Gomez aliwapumzisha Bernard Morrison, John Bocco na Medie Kagere kuwaingiza Hassan Dilunga, Chris Mugalu pamoja na Jonas Mkude.

Ushindi wa leo unawafanya Simba SC kukamilisha mipango yao ya kupata alama zote tisa katika mechi tatu za Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui FC, Kagera Sugar na leo Gwambina.

Hii ni mara ya kwanza msimu huu kwa Simba SC kukalia usukani wa ligi kuu ambapo inaongoza kwa tofauti ya alama moja huku wakiwa na michezo miwili mkononi.

SOMA NA HII  CHAMA, KAGERE NA MORRISON WAWALIZA MASHABIKI MBEYA...UONGOZI WATIA NGUMU ...WADAI UTARATIBU...