Home Simba SC SWALI, HIVI SISI HATUNA HATA CHAMA MMOJA?

SWALI, HIVI SISI HATUNA HATA CHAMA MMOJA?

WAKATI Simba inaingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa  Afrika kwa mara ya kwanza ikiivua Zamalek ubingwa wa Afrika, asilimia 95 ya kikosi chake kilikuwa ni cha wazawa.

Hii ilikuwa ni mwaka 2003, Simba ilicheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Zamalek kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) na kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na Emmanuel Gabriel “Batigol” ambaye alipokea krosi murua ya Ulimboka Mwakingwe.

Baada ya hapo, Simba wakasafiri kwenda Cairo, Misri na gumzo kubwa likawa kwamba watapoteza na zikiwa chache ni bao tano. Kumbuka, wakati huo Zamalek licha ya kuwa mabingwa wa Afrika, walikuwa ndiyo timu bora ya Bara la Afrika.

Mechi haikuwa nyepesi, Simba pamoja na kuwa na James Siang’a, pia walilazimika kuongeza nguvu ya makocha wengine kama Talib Hilal ambaye alisafiri kutoka nchini Oman kwenda kuungana na kikosi cha Simba.

Haikuwa mechi nyepesi, mwisho ikaisha Simba kulala kwa bao 1-0, likawa suala la mikwaju ya penalti, Kaseja akapangua penalti na Christopher Alex Massawe akamaliza kazi kwa kufunga mkwaju wa mwisho.

Nimeanzia mbali kidogo, lakini nilitaka kukupa picha tu kabla ya kuuliza maswali yangu wakati ukisoma makala haya nawe unaweza ukajiuliza mambo kadhaa na kupata kitu cha kujifunza, hiyo ndiyo nia yangu hasa.

Nimeizungumzia Simba ya mwaka 2003, lakini hata ningeizungumzia ile ya mwaka 1993 iliyoingia fainali ya Kombe la Caf, zaidi ungezungumzia wazawa wengi kama Hussein Marsha, George Magere Masatu, Edward Chumila na wengine wengi ambao walifanya vema wakati huo.

Simba sasa ndiyo timu inafanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kwa kifupi niseme hivi, hata TP Mazembe na AS Vita, wababe hawa wa DR Congo, hawako vizuri kama Simba kwa msimu huu.

Wakati Simba ikiwa na mwendo bora kama huo, furaha na faraja ni kubwa kwa Watanzania kwa kuwa ni Simba ya Tanzania. Lakini mimi nawaza tofauti, kikosi cha Simba kama utakipanga kama si nusu kwa nusu, basi zaidi ya nusu, wanaotegemewa watakuwa ni wachezaji wa kigeni.

Bado ninaweza kusema si jambo baya sana lakini bado ni baya, maana inapendeza zaidi kuona timu inafanya vema zaidi ikiwa na wachezaji wengi zaidi wazawa.

SOMA NA HII  LICHA YA KUIBUKA NA GOLI 5 ...HIZI HAPA REKODI ZA KIBABE ZILIZOWEKWA NA SIMBA JANA..

Tunakubali uwepo wa wageni kama sehemu ya kukuza mpira wetu, mnaweza kuwa na timu bora ya taifa kutokana na kuwa na timu imara. Timu zinapokuwa na wazawa wengi na zinafanya vema na hasa kimataifa, basi mna nafasi ya kufanya vizuri zaidi kupitia timu ya taifa.

Hauwezi kuwalaumu Simba, umeona mara kadhaa wamejaribu kuwachukua wachezaji wazawa, mfano mzuri washambulizi ambao waliamini watafanya vema na waliwapa nafasi lakini mwisho wakawaangusha, mfano mzuri ni Adam Salamba  Na baadaye Charles Ilamfya ambaye pia alishindwa kabisa.

Wakati mwingine najiuliza, hivi sisi Tanzania hatuna hata mchezaji mmoja mwenye uwezo kama wa Chama ambaye leo angekuwa anacheza pale katikati Simba na Taifa Stars?

Ukiachana na wachache kama Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, wachezaji wanaong’ara zaidi Simba ni wa kigeni. Hata kwa washambulizi, labda Bocco awe mzima lakini naye bado hajawa na uhakika wa namba.

Simba si jukumu lao kulazimisha kusajili wazawa tu, ni klabu yenye malengo yake na imejipanga kufanya jambo fulani. Hivyo mfano Ilamfya na Salamba wangefanya vema na wengine wa mfano wao, leo wangekuwa tegemeo Simba na Taifa Stars, lakini wakambwela.

Kuna wengi mfano wa Salamba na Ilamfya lakini kinachonishangaza, hivi hawaoni? Na kama wanaona hawana hata wivu wa maendeleo? Hadi lini itakuwa hivi na kwanini wale wachezaji wa zamani walifikia hadi hatua ya makundi wakiwa na wachezaji wachache sana wa kigeni. Kama iliwezekana kipindi hicho tukawa na wachezaji wengi wazawa na mafanikio yakapatikana, vipi washindwe sasa? Wachezaji wa kipindi hiki kwani wana tatizo gani?

Kuna kila sababu ya wachezaji wazawa kujifunza hili, walifanyie kazi na wajue wamelala, wamelegea na hawataki kupambana kufikia ndoto za kuwa tegemeo katika timu zote kubwa za Tanzania.

Kwingine wameweza, Afrika Kusini lakini Kaskazini mwa Afrika kama Algeria, Misri, Tunisia na Morocco, utaona timu zao zinafanya vizuri zaidi na wazawa ndio wanaotamba zaidi katika vikosi vyao, tujifunze angalau kupitia kwao. Wageni kufanya vizuri ni jambo zuri lakini wazawa kufanya vizuri zaidi ni jambo zuri zaidi ya vizuri.