UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa mipango yao kwa sasa ni kutwaa taji la Kombe la Shirikisho kwa kuwa uwezo wanao na nia ipo kwa kila mmoja.
Ushindi wa mabao 2-1 waliyopata mbele ya Polisi Tanzania umewapa nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.
Inaungana na Yanga, Simba ambao ni mabingwa watetezi, Dodoma Jiji pamoja na Mwadui FC ni baadhi ya timu ambazo zimetinga hatua hiyo.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa mpango mkubwa ni kupata ushindi kwenye mechi zao watakazocheza mpaka watakapotwaa ubingwa.
“Malengo yetu makubwa ni kuona kwamba tunapata kombe lolote lile ambalo ni kubwa katika mashindano ambayo tunayashiriki msimu huu na tuna amini itakuwa hivyo.
“Kwa kuwa tumetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho basi tutazidi kupambana ili kupata matokeo kwenye mechi zijazo,” amesema.