INTER Milan inayonolewa na Kocha Mkuu, Antonio Conte imefanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Italia, Serie A ikiwa na mechi nne mkononi jambo ambalo kwa sasa wanajivunia.
Kutwaa taji hilo kumekuwa kukitafsriwa na wachambuzi kwamba ule ufalme wa Juventus umeanza kumeguka taratibu kutokana na kuzidiwa ujanja na Inter Milan ambayo mshambuiaji wao mahiri ni Romelu Lukaku aliyejiunga na timu hiyo akitokea Klabu ya Manchester United.
Lukaku ametupia jumla ya mabao 21 katika mechi 33 ambazo amecheza na ana pasi tisa za mabao.
Mara ya mwisho Milan kushinda taji hilo ilikuwa ni zama za Jose Mourinho msimu wa 2010 hivyo wamepambana kurejesha heshima.
Conte ambaye alijiunga na Inter Milan msimu wa 2019 wengi walikuwa hawaamini kwamba anaweza kufanya makubwa ila mwisho wa siku amefanikiwa kuwatoa kimasomaso.
Kocha huyo amesema ushirikiano mkubwa pamoja na jitihada za wachezaji zimewafanya waweze kufikia mafanikio hayo.