NYOTA wa Azam FC, Mathias Kigonya ambaye ni kipa tegemeo ndani ya kikosi hicho kwa sasa anatibu majeraha yake ya bega ambayo ameyapata hivi karibuni.
Kigonya ni raia wa Uganda aliibuka Bongo kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akichukua nafasi ya mzawa, David Kissu ambaye kiwango chake kiliporomoka ghafla.
Kwa sasa Kissu bado yupo ndani ya Azam FC ila amekuwa hapati nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankwenwa amesema kuwa nyota huyo atakwenda kufanyiwa vipimo zaidi hospitali ili kujua tatizo lake.
“Kigonya kwa sasa anasumbuliwa na bega, tunatarajia kumpeleka hospitali kwa ajili ya kumfanyia uchunguzi zaidi ili apatiwe matibabu,” amesema.
Nyota huyo kwa sasa ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina.
Alijiunga na Azam FC akitokea Klabu ya Forest Rangers ya Zambia na kwenye mchezo dhidi ya Yanga alikaa langoni na kushuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Yanga 0-1 Azam FC.
Kwenye msimamo wa ligi, Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza jumla ya mechi 28.