UONGOZI wa Yanga umewashukuru mashabiki na wanachama ambao walijitokeza jana Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba na kusema kuwa wana bahati wapinzani wao wangefungwa nyingi.
Jana Mei 8 ulipaswa uchezwe mchezo wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga ilishindikana baada ya muda kubadilishwa kutoka saa 11:00 jioni mpaka saa 1:00 usiku jambo ambalo Yanga waligomea kwa kuwa halikufuata kanuni.
Kupitia ukurasa wao wa Instagram muda mfupi baada ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kueleza kwamba muda umebadilika kutokana na maagizo ambayo walikuwa wamepata, Yanga nao walijibu kwa kueleza kuwa ni kinyume na kanuni ya 15, (10).
Kanuni hiyo inasema:”Mabadiliko yoyote ya muda kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali,”.
Kutokana na kauli hiyo Yanga walipeleka timu saa 10:20 jioni kisha wakafanya mazoezi na kuondoka jumlajumla saa 11:39 huku wakipishana na Simba ambao waliingia saa 11:27.
Kupitia ukurasa wao wa Istagram Yanga wameandika namna hii:”Shukran kwa mashabiki, wanachama na wapenzi wa Young African Sc kwa kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba.
“Bahati yao maana walikuwa wanakufa nyingi, tulieni Wananchi, haki inaweza kuchelewa lakini haiwezi kupotea,”.