IMEELEZWA kuwa nafasi ya Kocha Mkuu wa Klabu ya Al Ahly, Pitso Mosimane ndani ya timu hiyo kwa sasa ipo mashakani kutokana na mwendo wa kusuasua wa timu hiyo.
Sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Zamalek kwenye mchezo wa ligi ambao ulikuwa ni wa dabi, inazidi kuongeza joto kwa kocha huyo kutokana na ushindani uliopo kwa timu hizo.
Pia ikumbukwe kwamba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 ilipokuja Bongo mbele ya Simba na Luis Miquissone kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza ikiwa nafasi ya pili katika kundi A ambapo vinara walikuwa ni Simba.
Bao la Salah Mohsen alilopachika dakika ya 70 lilikwama kudumu mpaka dakika ya 90 kwa sababu Ferjani Sassi alisawazisha dakika ya 80 na kufanya ubao kusoma 1-1.
Kwenye msimamo matajiri hao wa Misri wapo nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 19 na pointi zao kibindoni ni 41, watani zao wa jadi Zamalek ni namba moja na pointi 45 baada ya kucheza mechi 21.
Ina kazi ya kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo imetinga hatua ya robo fainali na itaanza kumenyana na Mamelodi Sundows, Mei 15.