KOCHA mkuu wa kikosi cha klabu ya Simba, Didier Gomes amefunguka kuwa kiungo mkabaji wa kikosi hicho, Jonas Mkude hakuwa na shida yoyote, bali alipewa ruhusa maalum ya kushughulikia masuala yake binafsi na ndiyo maana alikosekana kwenye mazoezi yao ya juzi.
Katika mazoezi hayo ya Jumatano yaliyofanyika kwenye viwanja vya Simba MO arena Bunju, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs, Mkude hakuwa sehemu ya wachezaji waliojifua kiasi cha kuzua gumzo la juu ya wapi alipo kiungo huyo.
Mkude alikuwa sehemu ya kikosi kilichoanza katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Afrika Kusini Jumamosi iliyopita ambapo Simba walikubali kipigo cha mabao 4-0, hivyo kuifanya kuwa na mlima mrefu wa kupata ushindi wa tofauti ya mabao matano ili kufuzu hatua ya nusu fainali.
Akizungumzia dharura ya Mkude, Gomes amesema: “Nyota wote wa kikosi chetu wako tayari kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho dhidi ya Kaizer Chiefs, isipokuwa kiungo mshambuliaji wetu, Jonas Mkude ambaye alipewa ruhusa maalum ya kushughulikia mambo yake binafsi, na atarejea atakapomaliza.”