WAWAKILISHI wa Tanzania malengo yao ya kutinga hatua ya nusu fainali yamekwama jana Mei 22 Uwanja wa Mkapa baada ya mlima wa mabao 4-0 waliyofungwa nchini Afrika Kusini kuwa ngumu kwao kuupanda.
Licha ya kuishia kufunga mabao 3-0 na kufanya jumla ya mabao kuwa Simba 3-4 Kaizer Chiefs, uongozi wa Simba umewapongeza vijana wao kwa jitihada walizozifanya.
Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imekuwa kikwazo kwa Simba ambayo iliweza kuonyesha uwezo mkubwa Uwanja wa Mkapa kukwama kusonga mbele na kutinga hatua ya nusu fainali.
Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema kuwa walipambana kwa hali na mali ila bahati haikuwa yao.
Mabao ya Simba yalifungwa na nahodha John Bocco ambaye alitupia mabao mawili dakika ya 24 na 56 na lile la tatu lilipachikwa na Clatous Chama dakika ya 86.
Kwa sasa Simba na Namungo ambao walikuwa ni wawakilishi wa Tanzania kimataifa wanabaki Tanzania kuendelea kupambana katika Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho.