Home Simba SC GOMES – TUNAELEKEZA JUHUDI KWENYE UBINGWA WA LIGI KUU

GOMES – TUNAELEKEZA JUHUDI KWENYE UBINGWA WA LIGI KUU



NYIE pigeni kelele tu. Lakini wao wala hawana hofu. Wanachosubiri ni siku hiyo kuwaonyesha soka linavyopigwa.

Ingawa Simba imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imetoa kauli ya ‘sisi na wao tu’ ikiwa na maana watakutana na wapinzani wao wa jadi Yanga iwe kwenye Ligi Kuu Bara au Kombe la Shirikisho la Azam na ndio watajua soka linavyochezwa wenyewe wakitetea ubingwa wa michuano yote hiyo msimu huu

Simba ilitwaa mataji yote mawili ya Ligi Kuu na Kombe la FA msimu uliopita.

Juzi Jumamosi Wekundu hao wa Msimbazi ilitolewa na Kaizer Chiefs hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya awali kufungwa ugenini mabao 4-0, kabla ya kushinda nyumbani mabao 3-0 na licha ya kutolewa imetamba wao ndio miamba ya soka sio tu Tanzania, bali Afrika nzima.

Simba imetoa kauli hizo kutokana na baadhi ya watu kuanza kuibeza, hivyo kuwakumbusha wanatakiwa kujifunza kutoka kwenye timu hiyo, bila kusahau wao hawajavunjika moyo wala kufadhaika kwani wamepambana kwa kiwango kikubwa.

Kwa sasa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu akili zao zote zimerudi kwenye ichuano hiyo mikubwa nchini na Kombe la Shirikisho la Azam wanakotamani kukutana na watani zao.

Simba ndio inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 61 sawa na Yanga zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku pia ikiwa na michezo minne ya viporo, huku Yanga ikiwa imeshacheza mechi 29 na wao 25.

Yanga kesho Jumanne itakuwa Uwanja wa CCM Kambarage dhidi ya Mwadui FC, huku Simba ikisubiri hadi keshokutwa Jumatano kuialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Uwanja wa Mkapa kwenye mechi za robo fainali za michuano hiyo.

Baada ya mchezo dhidi ya Dodoma, Simba itarudi kwenye viporo vyake na itacheza dhidi ya Namungo FC, Mei 29 kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa.

Kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes alisema kilichowaondoa kwenye michuano hiyo juzi, ni kushindwa kutumia nafasi nyingi za kufungwa walizozipata.

SOMA NA HII  MRITHI WA SVEN KUTAJWA RASMI NDANI YA SIMBA

“Shida ilianzia mechi ya kwanza, ugenini tulifungwa mabao mengi. Ni nadra sana kwenye hatua hii. Ilitokana na kucheza vibaya pamoja na kufanya makosa mengi ya kiulinzi. Hata hivyo, yalikuwa ni mabao mengi na hatukucheza vizuri kama tulivyotegemea.

“Baada ya kuangalia makosa yetu, tuliyafanyia kazi kama nilivyowahi kusema awali, tulifanikiwa kufanya vizuri mechi ya nyumbani ila tulishindwa kupata mabao tuliyoyahitaji. Tulipoteza nafasi nyingi za kufunga.

“Hata hivyo, nipo pamoja na wachezaji wote, kwani wanastahili pongezi kutokana na kujituma kwao na kuonyesha wanaweza,” alisema Gomes.

Baada ya kuiondoa Simba, Kwenye nusu fainali, Kaizer wanatarajia kukutana na Wydad Casablanca anayoichezea Mtanzania Saimon Msuva na timu hizo zilikutana awali kwenye hatua ya makundi na mechi ya kwanza iliyochezwa Morocco, Casablanca ilishinda 4-0 na marudiano Kaizer ilishinda 1-0.

Katika hatua nyingine, Gomes alisema licha ya wachezaji wake kupambana, hajafurahishwa na matokeo hayo, kwani yamevunja malengo yao ya kucheza nusu fainali.

“Bado nina deni ambalo natakiwa kulilipa Simba pamoja na kuweka alama kwenye mashindano haya kwa kuvuka hatua hii tuliyofika mara ya pili mfululizo.

“Sasa nguvu zetu tunakwenda kuweka katika mashindano ya ndani na kuchukua kila kombe lililopo mbele yetu kutokana na ubora wa kikosi kilivyo naona tuna kila sababu ya kufanya hivyo.” alisema Gomes.