Home Simba SC SIMBA KAMILI KUIVAA KAGERA SUGAR LEO KWA MKAPA

SIMBA KAMILI KUIVAA KAGERA SUGAR LEO KWA MKAPA


 UONGOZI wa Simba umeweka wazi kwamba upo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 16 bora dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, saa 1:00 usiku.

Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes, raia wa Ufaransa ni mabingwa watetezi ambapo walitwaa taji hilo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC, Uwanja wa Nelson Mandela.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Patrick Rweyemamu, Meneja wa Simba alisema kuwa maandalizi yapo sawa licha ya kwamba jana, (Juzi) kushindwa kufanya mazoezi kutokana na mvua.

“Kila kitu kipo sawa na tunaamini kwamba mchezo utakuwa mgumu ila tupo tayari na tunahitaji ushindi. Jana, (Juzi) tulishindwa kufanya mazoezi kwa ajili ya hali ya hewa ya mvua ila nina amini leo, (jana) tutafanya mazoezi ya mwisho.

“Kwa upande wa wachezaji ambao wataukosa mchezo huo kwetu sisi hakuna majeruhi hivyo ni jukumu la mwalimu kujua nani atamtumia kwenye mchezo wetu,” alisema.

Ni wachezaji wawili ambao hawatatumika katika mchezo wa leo ambao ni beki Ibrahim Ame huyu amefungiwa na Kamati ya Masaa 72 mechi tatu pamoja na Francis Kahata ambaye yupo kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza aliliambia Championi Jumamosi kuwa maandalizi yalikamilika ila alipewa mapumziko kuelekea nchini Kenya kwa ajili ya msiba wa mama yake mzazi.

“Timu nimeacha imekwenda Dar ila mimi ninaelekea Kenya kwa ajili ya msiba, ninashukuru kwa ajili ya pole ambazo nimepewa hivyo nina amini kwamba kila kitu kitakuwa sawa kwa kuwa mipango ilikuwa imekamilika, ” alisema Baraza.

Kagera Sugar inakumbuka kwamba msimu uliopita ilipoteza hatua ya 16 bora kwa kufungwa mabao 2-1 mbele ya Yanga na mchezaji wao Awesu Awesu alionyeshwa kadi nyekundu hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari.

SOMA NA HII  BAADA YA KUMCHUKUA CHAMA KIBABE..IBENGE NA TIMU YAKE WAMMEZEA MATE MANULA..