Home Habari za michezo A-Z KILICHOIPONZA SIMBA JANA MBELE WA YA TZ PRISONS….REKODI YA BECHIKHA YATIBUKA…

A-Z KILICHOIPONZA SIMBA JANA MBELE WA YA TZ PRISONS….REKODI YA BECHIKHA YATIBUKA…

Habari za Simba leo

MABAO mawili ya straika tegemeo wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula aliyofunga jana jioni kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro yamemtibulia kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha katika Ligi Kuu ya Bara wakati Mnyama akifumuliwa mabao 2-1.

Mbangula aliyewahi kuitungua pia Simba mwaka 2020 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa alifunga mabao hayo kila kipindi na kutoa kipigo cha Mnyama ikiwa ni cha pili msimu huu baada ya kile cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga katika mechi ya Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana.

Simba iliuchagua Jamhuri kama uwanja wa nyumbani baada ya kufungiwa kwa Uhuru iliyokuwa inautumia kisha kuukacha Azam Complex, iliyotumia kwa mechi za ASFC unaotumiwa na pia Azam, KMC , JKT Tanzania na Yanga, na jana ilikuwa ikicheza kwa mara ya kwanza hapo na kukumbana na kipigo hicho kilichomtibulia Benchikha.

Kocha huyo alikuwa hajapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu tangu aajiriwe Novemba mwaka jana kuchukua nafasi ya Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ lakini Mbangula alifunga bao la kwanza sekunde chache kabla ya mapumziko, kisha kuiongeza jingine dakika ya 62 na kuizima Simba iliyowakosa baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza.

Katika mechi hiyo iliyokuwa kali na yenye ushindani, huku wageni wakionekana kupania, Simba iliwakosa Sadio Kanoute, Fondoh Che Malone waliokuwa jukwaani, huku Mohammed Hussen Tshabalala na Saido Ntibazonkiza wakianzishwa benchi na lango akianza Aishi Manula aliyetunguliwa mabao hayo yaliyotokana na uzembe wa safu nzima ya ulinzi ya timu hiyo.

Prisons iliyokuwa ya kwanza kuingia Uwanja wa Jamhuri jana ikiwasili saa 8:13 mchana kisha kufuatiwa na Simba iliyoingia uwanjani saa 8:34 mchana, ilijikuta ikimaliza dakika za lala salama ikiwa pungufu baada ya kiungo wake, Mussa Haji kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyosindikizwa na nyekundu kutoka kwa mwamuzi Nassor Mwinchui baada ya kumchezea madhambi, Saido dakika ya 88.

Kutolewa kwa mchezaji huyo kuliipa nafasi kwa Simba kucharuka zaidi kusaka bao na kufanikiwa kuandika dakika moja baadae kupitia kwa Fabrice Ngoma lililokuwa ni bao lake la pili msimu huu.

Licha ya kipigo hicho, Simba itajilaumu yenyewe kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi kutoka kwa nyota wake katika kipindi, ikiwamo ile ya Freddy Michael aliyebaki na kuipa wa Prisons, Yona Amos katika kipindi cha kwanza, huku Pa Omary Jobe naye akishindwa kutupia mpira nyavuni katika kipindi cha pili, mbali na kosa kosa za Kibu Denis, Clatous Chama na Saido aliyeingia kipindi cha pili.

Matokeo ya hayo yameifanya Simba kusalia nafasui ya tatu ikiwa na pointi 36 naada ya mechi 16, huku Prisons ikiingia katika Nne Bora kwa kufikisha pointi 27 ikitoka nafasi ya sita na Mbangula kufikisha jumla ya mabao saba katika Ligi Kuu kwa msimu huu akiwa ndiye kinara wa timu hiyo.

Mbangula, pia aliwahi kuitungua Simba bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga Oktoba 2020 na huu ni ushindi wa kwanza wa Prisons nyumbani kwa Simba tangu mwaka 2012, lakini ni wa pili ndani ya misimu mitatu iliyopita tangu ilipoifunga Simba pia 1-0 kwa bao la Benjamin Asukile mechi iliyopiga Juni 26, 2022.

SOMA NA HII  GAMONDI AFUNGUKA HAYA KUHUSU MCHEZO WAO NA SINGIDA FG