Home Yanga SC YANGA: ISHU YA MWAKALEBELA, TUNATAKA HAKI NA SI UONEVU

YANGA: ISHU YA MWAKALEBELA, TUNATAKA HAKI NA SI UONEVU

 


LICHA ya kufikia makubaliano ya baadhi ya mambo kati ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), na klabu ya Yanga katika vikao vyao pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, bado shauri la rufani ya makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela limeonekana kuwa gumu ambapo kwa sasa limepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya bodi ya Ligi.

Aprili 2, mwaka huu Mwakalebela alikutana na rungu la kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano na faini ya Shilingi Milioni 5, baada ya kukutwa na hatia ya kutoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kuchochea mashabiki, wanachama na wapenzi wa Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia mpira wa miguu.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa habari wa kikosi cha klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema: “Sisi tuliipokea ile taarifa ya adhabu ya Makamu Mwenyekiti na kitu cha kwanza ni kuwa tuliipinga kumaanisha ile adhabu hatukukubaliana nayo, lakini pili tulikata rufaa ambayo ilisikilizwa na kamati ya rufani, wao TFF wana mamlaka ya kutangaza nini kimetokea.

“Lakini suala la mwenyekiti na masuala mengine kama tisa ilikuwa miongoni mwa masuala muafaka ambayo Yanga tulikubaliana na TFF, katika vikao vyetu tulivyofanya na Wizara pamoja na TFF, kwahiyo tunaamini TFF watakuwa na majibu mazuri kuhusiana na hilo.

“Sisi kama klabu ya Yanga tumekata rufaa na tunasubiri majibu ya rufaa hiyo, lakini kwa sasa tunaendelea na taratibu nyingine ili kuhakikisha yale yote ya msingi ambayo Yanga wanastahili kuyapata kwa mujibu wa taratibu, Sheria na kanuni na si uonevu yanafanyika.”

Naye Ofisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema: “Suala la Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kwa sasa lipo chini ya kamati ya nidhamu ya Bodi ya Ligi na kama kutakuwa na majibu yoyote basi mtapewa taarifa.”

SOMA NA HII  SIKU MOJA BAADA YA KUTUA BONGO.....GAMONDI AMCHOMOA GUEDE YANGA....