KOCHA Didier Gomes amewaambia mashabiki wa Simba SC wajiandae mapema kusherekea ubingwa wa ligi kuu ,kwani kazi iliyobaki ni kidogo tu.
Simba wanahitaji pointi 13, katika mechi zao nane walizobaki nazo ili kutangaza ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.
Gomes alisema anajua kwamba wanaweza kuzipata pointi hizo kufikia mwisho wa msimu lakini hataki kusubiri hadi wakati huo.
“Tulianza kazi ya kutafuta pointi hizo katika mechi dhidi ya Namungo ambazo tulifanikiwa wakati huo huo tunaenda ugenini tena Mwanza kuwavaa Ruvu Shooting, nina imani tutachukua pointi nyingine,” alisema Gomes na kuongezea;
“Baada ya hapa tutakwenda ugenini tena kucheza na Polisi Tanzania. Licha ya changamoto za viwanja na mechi za ugenini ambazo tunakutana nazo tutachukua pointi tatu kutokana na wachezaji wangu kuniahidi watajitolea mwanzo mwisho.
“Tutarudi nyumbani kucheza mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Yanga ambazo tukishinda zote malengo yetu ndio tutakuwa tumeyakamilisha kwa kutangazwa mabingwa na hilo linawezekana kwetu,” aliongeza kocha huyo.
Simba msimu huu wamefungwa mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting ambao watacheza nao Juni 3, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Gomes alisema; “Shooting ni moja ya timu nzuri katika ligi hata katika mechi ya kwanza waliyotufunga walicheza vizuri ila awamu hii tutakuwa imara zaidi yao.”
Katika mechi hiyo ya mzunguko wa kwanza wakati Simba wanafungwa kocha mkuu alikuwa, Sven Vandenbroeck ambaye hayupo kwa sasa.
Simba kama watapata pointi 13, katika mechi tano kama ambavyo wameeleza maana yake watafikisha pointi 77 na kuwaacha wapinzani wao Yanga na pointi 76 kama watashinda mechi zao nne watakazobakiwa nazo.
Kocha wa makipa wa Simba, Milton Nienov alisema; “Wachezaji wetu wamekuwa na morali pamoja na ushindani wa kutosha jambo ambalo linatusaidia kupata matokeo mazuri hata katika michezo migumu zaidi kama ule wa Namungo.”
“Ambalo naliona kutokana na uhalisia wa ubora wa kikosi chetu tunanafasi ya kuwa mabingwa mapema tukiwa na mechi mkononi.”