HATIMAYE beki wa kulia wa AS Vita na timu ya Taifa ya DR Congo, Djuma Shabani, amefunguka kuwa yupo tayari kujiunga na Yanga ambayo wapo katika mazungumzo ya mwisho kukamilisha dili lake.
Beki huyo anasifika kuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia pamoja na kushambulia kwa kasi jambo ambalo limewashawishi viongozi wa Yanga juu ya kumsajili.
Akizungumza na Spoti Xtra moja kwa moja kutoka DR Congo, beki huyo alikiri yupo katika mazungumzo na Yanga juu ya kujiunga na timu hiyo.
“Ni kweli tupo katika mazungumzo na Yanga, uongozi wangu nimewaeleza ninachohitaji, kama Yanga watakubali basi nitajiunga nao, sitakuwa na shida juu ya hilo kwa kuwa mpira ndio kila kitu kwangu. Uongozi wangu unafahamu kila kitu kuhusu hili, tusubiri tuone,” alisema beki huyo.
Spoti Xtra liliutafuta uongozi wa mchezaji huyo ambaye yupo chini ya usimamizi wa Kampuni ya Bro Soccer Management, meneja wake Faustino Mukandila, alisema: “Tupo katika makubaliano ya mwisho na Yanga ya kumsajili Djuma Shabani, katika hili hakuna kingine ambacho naweza kukuambia, labda taarifa za kukamilika kwa usajili wake kujiunga na Yanga.”