NI rasmi kwamba Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji yuko njiani kurejea Jangwani na Mwanaspoti limejiridhisha kwamba amelipia kadi yake ya uanachama Ijumaa iliyopita Jijini Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Manji ambaye bado hajataka kuzungumza chochote rasmi, alimtuma mmoja wa wasaidizi wake kulipia mchakato huo kimyakimya na huenda akaibuka kwa sapraizi kubwa Jangwani kwenye mkutano Mkuu wa Jumapili.
Manji alirejea nchini hivi karibuni na kuibua furaha kwa mashabiki wa Yanga huku baadhi ya viongozi wakilidokeza Gazeti la Mwanaspoti kwamba wamezungumza naye akasema anaweka kwanza ishu zake freshi kisha ataangalia namna gani ya kuwekeza Jangwani.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata Jangwani ni kwamba Manji ambaye alijiuzulu nafasi ya Uenyekiti Mei 22, 2017 Ijumaa iliyopita alilipia kadi yake ya uanachama ada ya mwaka mzima.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba Manji atahudhuria kikao cha wanachama kitakachofanyika Jumapili ijayo Jijini Dar es Salaam.
Kwenye stakabadhi ambazo gazeti la Mwanaspoti imezinasa ni kwamba Manji amelipia Sh12,000 ambayo ni ada ya mwaka mzima klabuni hapo ili mwanachama awe hai kikatiba.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba Manji atahudhuria mkutano huo kama sehemu ya kuwasalimia wanachama wenzie na kujua kiundani kuhusiana na mchakato wa mabadiliko.
Habari kutoka ndani ya uongozi zinasema kwamba wamepania kuhakikisha matajiri watatu, Ghalib Said (GSM), Rostam Aziz na Manji wanawekeza ndani ya Yanga katika mfumo mpya wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu.
Katika mkutano wa Jumapili ijayo moja ya ajenda ni kupitia mapendekezo ya marekebisho ya katiba na taratibu za Yanga na hapo ndani ishu ya mabadiliko na hisa itakapojadiliwa. Yanga imepania kufanya mabadiliko makubwa ya kiuendeshaji na kuwa ya kisasa zaidi na kuruhusu matajiri wengi kuweka fedha zao.