MCHAKATO wa uchaguzi kwa sasa bado unaendelea ambapo leo majina ya waliopenya hatua ya kugombea nafasi ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) inatarajiwa kuwa hadharani baada ya jana mipango kutokwenda sawa.
Kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya uchaguzi wa TFF Juni 28-29 ni siku ya mwisho kukamilisha mchakato huo na leo Juni 29 itakuwa ni siku ya kutangaza na kubandika kwenye mbao za matangazo matokeo ya awali ya usaili na itafanywa na Kamati ya Uchaguzi TFF.
Uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 8 ikiwa chini ya Kimoni Kibamba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya TFF zimeeleza kuwa mchakato huo jana ulikuwa kwenye maandalizi ya mwisho hivyo leo zoezi litakamilika.
“Jana ilikuwa ngumu kukamilika kwa kuwa kwa mujibu wa kalenda ni Juni 28-29 ni siku za kubandika matokeo hivyo leo uhakika, ilieleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa nafasi ya Urais ni wagombea watatu walipitishwa kwenye mchujo wa awali ambao ni Evans G Mgeusa, Hawa Mniga na Wallace Karia ambaye anatetea kiti chake. Huku kwa upande wa wajumbe wakiwa ni 17 katika kanda 6.
Makamu Mwenyekiti wa Uchaguzi wa TFF, Benjamin Kalume alisema kuwa watasimamia haki katika uchaguzi huo kwa mujibu wa kanuni.