Home news ALLY MAYAY, OSCAR OSCAR WAKATWA URAIS TFF,

ALLY MAYAY, OSCAR OSCAR WAKATWA URAIS TFF,


Wagombea 10 wakiwamo watatu waliokuwa wakiwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF) wameenguliwa kwenye mchujo wa awali.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Benjamin Karume amesema wagombea hao wameenguliwa kwa kutokidhi vigezo vya kikanuni.

Amesema kwenye nafasi ya urais walioenguliwa ni Ally Mayay, Oscar Oscar na Ally Salehe.

“Mayay amepata mdhamini mmoja kati ya watano waliotakiwa kikanuni huku Oscar na Salehe wakikosa, udhamini kabisa,”

Amesema kwenye ujumbe walioenguliwa ni Liston Katabazi,  Jimmy ‘Kindoki’ Msindo, Saady Khimji, Thabit Kandoro, Denis Manumbu, Joseph Ngunangwa na Mrisho Ramadhan kutoka kanda namba moja mpaka namba nne huku wagombea wa kanda namba tano na sita wote wamepenya kwenye mchujo wa awali.

Amesema wagombea hao hawakukidhi takwa la kikanuni la wagombea  kuwa na mdhamini angalau kuanzia mmoja kwenye nafasi ya ujumbe.

“Wapo ambao wamedhaminia na klabu, kanuni zilitaka wadhamini wawe wa mikoa kwenye ujumbe,” amesema.

Alipoulizwa idadi ya wagombea waliojitokeza na mikoa kutokidhi mahitaji ya wagombea wote, Karume alisema ipo mikoa iliyokosa watu wa kuwadhamini.

“Siwezi kuikumbuka ni ipi, lakini kuna mikoa haikudhamini mtu,” amesema na kuongeza.

“Tunaelekea kwenye usaili na pingamizi, tunatarajia watakaoweka pingamizi zitakuwa sahihi na kamati haitomuonea wala kumpendelea yoyote,” amesema.

Amesema baada ya mchujo wa awali, nafasi ya urais sasa imesalia na wagombea Hawa Mniga, Wallace Karia na Evans Mgeusa.

SOMA NA HII  SIMBA WAIFANANISHA AL AHLY NA ZAMALEK