Home Yanga SC BAADA YA MKUTANO: WACHEZAJI YANGA WALA KIAPO KUISAMBARATISHA SIMBA

BAADA YA MKUTANO: WACHEZAJI YANGA WALA KIAPO KUISAMBARATISHA SIMBA


WAKATI wakiwa na furaha ya kilichofanywa juzi kwenye mkutano mkuu wa mwaka, wanachama na mashabiki wa Yanga wamejazwa upepo, baada ya nyota wao, kuwaahidi kuwa Julai 25, watawapa raha kwa kuwafumua Simba kwa madai wanaamini watani wao wanapigika sana!

Wachezaji wa Yanga waliotoka kuwafumua Biashara United kwa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC), wamesema kukutana kwao na Simba katika mechi ya fainali ya michuano hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Wakizungumza kwa muda tofauti na gazeti la Mwanaspoti, mastaa wa Yanga walisema hawana kigugumizi kutoa kauli za kishujaa, kwa vile hawahofii kukutana na Simba kwenye fainali, kwani wapo kamili gado na watapigana vita vya ushindi wa kulipeleka taji Jangwani.

Jeuri ya mastaa hao, inatokana na Yacouba Songne kufunga bao lililoipeleka fainali kwa mara ya kwanza tangu 2016 walipotinga na kushinda kwa kuinyoa Azam FC mabao 3-1 wakisisitiza wanaitaka tiketi ya CAF kwa nguvu zao wenyewe.

Beki wa kushoto, Adeyum Saleh alisema haikuwa kazi nyepesi kuisulubu Biashara na kwamba ushindani wa mechi hiyo, ndiyo umewaongezea morali ya kutohofia kukutana na Simba katika kwa kujiapiza lazima kieleweke.

Adeyum alisema wana dhamira, nguvu, ari ya kutimiza ndoto hiyo kuwa kwenye uhalisia ambao utakuwa niwamashabiki wao kuwapokea taji hilo kwa shangwe kama walivyofanya ndani ya mwaka huu kulichukua la Kombe la Mapinduzi.

“Sio kwamba hatujui kwamba fainali itakuwa ngumu, lakini penye ugumu ndipo itakapoonekana bidii yetu, tumedhamiria kulichukua taji hilo, iwe kwenye mvua ama jua tupo tayari kupambana kama jeshi la Yanga,” alisema.

Naye winga wa timu hiyo, Deus Kaseke alisema dhamira yao ni kuona wanawapa furaha mashabiki wao kwa kuwapelekea taji la ASFC na kwamba wanatambua ushindani utakuwa mkali, lakini mwenye kisu kikali ndiye atakayekula nyama.

“Fainali itakuwa ngumu na hiyo ndio maana halisi ya kuwania taji kwamba anayeupatia vyema mchezo ndiye anacheka, tunahamasishana na mashabiki watuunge mkono ili kufanikisha hilo,” alisema Kaseke mwenye mabao sita katika Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  NYOTA HAWA WATATU WA YANGA KUIKOSA RIVERS UNITED

Kiungo fundi wa mpira, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alisema wanatambua wapo vitani na wanahitaji kurejea nyumbani wakiwa na sura za kishujaa, zitakazokuwa zinawapa tabasamu mashabiki wao kumaliza msimu huu kwa kicheko.

Fainali ASFC, Julai 25, 2021, Saa 9:30 Alasiri Lake Tanganyika, Kigoma.