Home Simba SC HII HAPA MITIHANI MINNE ILIYOSALIA YA GOMES NDANI YA SIMBA

HII HAPA MITIHANI MINNE ILIYOSALIA YA GOMES NDANI YA SIMBA


MASHABIKI wa Simba kwa sasa roho zao kwatu! Tayari wana uhakika wa chama lao kubeba taji la nne mfululizo la Ligi Kuu Bara, huku wakihesabu saa tu kabla ya kujua hatima yao katika michuano ya Kombe la Shirikisho loa Azam (ASFC) wakati jioni ya leo wakicheza na Azam FC.

Simba inavaana na Azam katika mechi ya nusu fainali itakayopigwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea na kama watapenya hapo watakuwa na nafasi nyingine ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo, kwani msimu uliopita waliupata kwa kuwanyoa Namungo mjini Sumbawanga, Rukwa.

Kwa sasa Simba wanatambia kikosi kipana chenye wachezaji wa viwango vya juu sambamba na ufundi na umahiri wa Kocha Mkuu Didier Gomes ambaye mashabiki wanamtabiria kama atadumu Msimbazi muda mrefu anaweza kuwapa mafanikio makubwa zaidi.

Kwa muda mfupi aliokaa na timu hiyo, Gomes ameonyesha ubora wake ingawa bado ni mapema kwake kutembea kifua mbele kutokana na kazi kubwa aliyonayo kufikia rekodi kadhaa zilizowekwa na watangulizi wake.

Tayari ameshaifikia rekodi iliyowekwa na Patrick Aussems aliyeifikisha Simba katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kama ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, kuna kila dalili akamfikia Sven Vanderbroeck.

Lakini sasa, Gomes anatakiwa kupambana zaidi ili aweze kuvunja rekodi iliyoachwa na Dragon Popadic, kocha mzungu aliyedumu Msimbazi kwa muda mrefu kuliko makocha wengine kutoka Ulaya, akifanya hivyo kuanzia mwaka 1994 – 1996.

Ndani ya misimu hiyo kama mitatu, Popadic aliweka rekodi ya kutwaa mataji saba – idadi ambayo haijawahi kufikiwa na kocha yeyote. Alibeba mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Kagame mara mbili, Ligi Kuu ya Muungano mara mbili na Kombe la Nyerere.

Gazeti la Mwanaspoti linakuletea mambo manne ambayo akiyafanyia kazi Gomes anaweza kuandika rekodi iliyowashinda wenzake wengi wa kigeni waliopita Msimbazi kwa miaka ya hivi karibuni.

FAINALI ZA CAF

Simba imekuwa bora hakuna anayeweza kupinga kwenye hilo, kwani rekodi zinaonyesha katika misimu mitatu mfululizo imetwaa taji la Ligi Kuu Bara na sasa inajiandaa kubeba la nne kutokana na mwenendo wake mzuri ilionao.

Gomes anatakiwa kuivunja rekodi ya Aussems aliyoifikia msimu huu kwenye michuano ya CAF kwa kufika nusu fainali kama ilivyowahi kufikiwa mwaka 1974 wakati michuano hiyo ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika.

SOMA NA HII  BAADA YA MANENO MANENO KUWA MENGI KUHUSU KOCHA MPYA...UONGOZI SIMBA WAIBUKA NA TAMKO HILI...

Kutokana na ubora wao kuendelea kupanda kadri wanavyoshiriki mashindano hayo ya kimataifa, endapo kocha Gomes atadumu Msimbazi na kuipambania timu hiyo kuifikisha nusu au fainali, atakuwa ameingia kwenye kitabu cha kumbukumbu na kujiandikia historia ya kipekee.

MATAJI YOTE YA NDANI

Siyo jambo geni kwa Simba kwani lilishawahi kufanyika hapo nyuma, lakini ni muda sasa tangu lifanyike na sasa wapo katika hatua nzuri za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na pia kushiriki Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kama alivyofanya Sven aliyetwaa na Ngao ya Jamii.

Gomes ana nafasi kubwa ya kutwaa mataji hayo endapo ataendeleza ubora wa kikosi chake cha sasa na kutoruhusu kuuzwa kwa nyota wengi wa kikosi cha kwanza, lengo ni kuhakikisha hatapata tabu ya kuanza kupanga upya kikosi. Na kama ataendeleza moto atakuwa na kazi ya kubeba Ngao ya Jamii kwanza, kisha kukomba mataji mengine likiwamo Kombe la Mapinduzi, ikiwezekana.

KUPIGA MTANI NJE NDANI

Kwa soka la Tanzania mashabiki wa Simba na Yanga wapo tayari kukosa taji hata misimu yote, lakini furaha yao ni kuona chama lao linapata ushindi kwenye mechi ya watani.

Ni Abdallah Kibadeni pekee mwenye rekodi ya kuifunga Yanga nje ndani akiwa kocha mkuu wa Simba kwa miaka ya karibuni. Rekodi hiyo haijavunjwa hadi sasa, na endapo Gomes ataweza ataingia kwenye kumbukumbu. Kianzio chake ni mechi ya Julai 3, wakati timu hizo zitakaporudiana kwa msimu huu.

Mechi ya awali Simba ikiwa chini ya Sven matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.

MSIMU BILA KUPOTEZA

Mara ya mwisho Simba kutwaa taji la Ligi Kuu Bara bila kupoteza ilikuwa msimu wa 2009-2010, enzi hizo ikiwa chini ya Patrick Phiri kutoka Zambia aliyekuwa ametoka kumpokea Mserbia Cirkovic Milovan.

Tangu wakati huo Simba haijawahi kurudia tena rekodi hiyo iliyowahi kufikiwa pia na Azam waliotwaa taji lao la kwanza na la pekee msimu wa 2013-2014.

Pamoja na ubora wa kikosi alicho nacho Gomes hadi sasa tayari ameruhusu kufungwa mechi mbili, hivyo kama atataka kufikia rekodi hiyo anatakiwa kujipanga msimu ujao endapo ataendelea kuaminiwa na kuachiwa timu tena, kisha kulipanga jeshi lake kufikia rekodi hiyo.