Home news BAADA YA MANENO MANENO KUWA MENGI KUHUSU KOCHA MPYA…UONGOZI SIMBA WAIBUKA NA...

BAADA YA MANENO MANENO KUWA MENGI KUHUSU KOCHA MPYA…UONGOZI SIMBA WAIBUKA NA TAMKO HILI…


WAKATI baadhi ya mashabiki wa Yanga wakikejeli ujio wa Kocha Mpya wa Simba, Pablo Franco, mabosi wa Msimbazi wamevunja ukimya na kusema wapinzani wao wakae kwa kutulia kwani fundi huyo anakuja kuwanyamazisha ndani ya Ligi Kuu Bara na michuano mingine ya kimashindano nchini.

Uongozi huo wa Simba, umetamba kuwa haujutii kumuajiri kocha Pablo asiye na uzoefu wa soka la Tanzania na Afrika kijumla, lakini wanaamini atawapa mafanikio makubwa katika mashindano itakayoshiriki nje na ndani ya Tanzania.

Pablo alitambulishwa rasmi na Simba, Jumamosi iliyopita na Jumatano ya wiki hii alitua nchini na kuanza kibarua cha kuinoa timu hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza na jana jioni alikuwa akiongoza jeshi lake kutesti mitambo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Cambiaso.

Licha ya rekodi zake kuonyesha amefundisha soka Ulaya, Asia na Mashariki ya Mbali, lakini mabosi wa Msimbazi wamesema wanaombeza kwa sasa watanyamaza wenyewe mara atakapoanza kuiongoza timu hiyo katika Ligi Kuu na michuano mingine itakayoshiriki. 

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi alisema hawana shaka na ubora na uwezo wa Pablo na wanaamini utakuwa chachu kwao kufanya vizuri na suala la uzoefu wa soka la Afrika hawadhani litakuwa changamoto kubwa kwake.

“Franco (Pablo) ni kocha mwenye wasifu mkubwa sana na haikuwa rahisi kumpata na hadi uamuzi wa kuwa naye unachukuliwa kuna mambo mengi tumeyazingatia hatukumchukua kwa bahati mbaya.”

“Suala la kutokuwa na uzoefu wa soka la Afrika sidhani kama ni tatizo kwani iko mifano mingi ya makocha ambao walikuja kama yeye na wakafanya vizuri. Simba ni timu kubwa Afrika na inahitaji kuwa na kocha mkubwa na ndio maana tumemleta Franco ambaye tunaamini ataleta mafanikio makubwa katika timu,” alisema Mulamu.

Mulamu, alisema wamejiridhisha vya kutosha juu ya ubora wa kocha huyo na hawana shaka naye hivyo mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kuwa na wasiwasi wowote juu ya Franco na badala yake wanatakiwa kumpa ushirikiano mkubwa yeye na timu ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea.

SOMA NA HII  YANGA KUMEKUCHA...WAZIDI KUMIMINA MIZAWADI YA 'KRISMASI BOXING DAY'..SAFARI HII KICHEKO TU..

 Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo katika Ligi Kuu, Mulamu alisema kuwa sio mbaya na wana matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya tano mfululizo.

“Ligi ndio kwanza imechezwa raundi tano na tofauti ya pointi baina yetu na wanaoongoza ligi ni nne tu. Bado nafasi ya kutwaa ubingwa tunayo ingawa tunafahamu msimu huu ushindani umeongezeka.

Tuna imani timu itaimarika na itakuwa bora zaidi katika michezo inayofuata na ndio maana tumehakikisha tumelishughulikia haraka suala la kocha,” alisema Mulamu.

Iko mifano mingi ya makocha ambao walienda kuzifundisha timu pasipokuwa na uzoefu na soka la nchi au mazingira ya bara la Afrika na wakafanikiwa

Mfano wa makocha ambao waliwahi kuja Afrika wakiwa hawafahamu lolote kuhusu mazingira ya Afrika na hawana uzoefu na soka la huku na wakafanikiwa kufanya vyema ni Manuel José de Jesus Silva aliyewahi kuinoa Al Ahly hapo nyuma.

Kocha huyo alikuja Afrika akitokea Ureno na alifanikiwa kushinda mataji 20 akiwa na timu hiyo ya Misri ikiwemo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwaka 1999, Cameroon ilimuajiri kocha Pierre Lechantre ambaye hakuwa na uzoefu wowote wa soka la Afrika na pia hakuwahi kufundisha timu yoyote ya Taifa wala klabu kubwa duniani lakini akaja kuiongoza timu hiyo kutwaa taji la Mataifa ya Afrika mwaka 2000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here