Home news IMEFICHUKAAH..YANGA WAONGOZA ‘KUTOA PESA’ ILI WASHINDE …SIMBA, AZAM NAO WAMO..RIPOTI KAMILI HII...

IMEFICHUKAAH..YANGA WAONGOZA ‘KUTOA PESA’ ILI WASHINDE …SIMBA, AZAM NAO WAMO..RIPOTI KAMILI HII HAPA..


KIKOSI cha Yanga kimerejea jijini Dar es Salaam jana mchana, huku Kocha wake, Nasreddine akisisitiza kazi itaendelea ilipoishia, lakini mastaa wa timu hiyo wakiogolea noti baada ya kuvuna mkwanja wa maana kupitia mechi zao tano za awali za Ligi Kuu Bara.

Yanga ilikuwa visiwani Zanzibar kwa kambi ya muda mfupi na kucheza mechi mbili ambazo zote ikishinda ikianza kwa kuifumua Mlndege kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Heritier Makambo, kisha juzi usiku wakaipiga KMKM kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Jesus Moloko na Fiston Mayele.

Kasi ya ufungaji mabao ya nyota hao wa Yanga imewashtua timu pinzani wakati Ligi Kuu Bara itakaporejea tena Ijumaa ijayo na jana wakati wakitua Dar kutokea Unguja, kocha Nabi alisisitiza, kambi imemsaidia kwa mengi na sasa wanaenda kuendelea pale walipoishia ligi iliposimama.

Lakini hali ikiwa hiyo, unaambiwa mbali na ubora wa wachezaji wao, lakini Simba na Yanga zimeonyesha kuwa imara pia upande wa bonasi inayopelekea kuongeza ushindani mkubwa kwenye vikosi vyao ikifuatiwa na Azam FC.

Unaambiwa kwenye mechi hizo tano za awali, mastaa wa Yanga walivuna fedha za kutosha kutoka kwa mabosi wao ambao hutyoa bonasi kila timu ikitoka na ushindi.

Licha ya kwamba Simba na Yanga wanapokutana wachezaji hupewa bonasi kubwa kulingana na mechi yenyewe ilivyo, pia timu hizo zinapokutana na Azam dau la wachezaji katika mgawanyo wa bonasi linakuwa juu ukilinganisha na pale na wanachezaji na timu nyingine.

Hata hivyo, licha ya Simba na Yanga kupata bonasi ya Sh20 milioni kila wanaposhinda mechi za ligi, pesa hiyo imekuwa ikiongezeka zaidi pindi timu hizo zinapokutana zenyewe kwa zenyewe katika mchezo wa watani wa jadi kwani husababisha viongozi kuahidi donge nono zaidi kuanzia Sh100 milioni na kuendelea.

Kwa mechi hizo tano za awali, kwa utaratibu wa Yanga wa kutoa bonasi ya Sh20 milioni kwa kila mechi wanayoshinda, maana yake vijana wa Jangwani wamevuna Sh100 milioni, mbali na chambichambi nyingine kutoka kwa wadau wa klabu hiyo.

Pia wachezaji wa Simba wameendelea kunufaika zaidi katika mechi zao za kimataifa kwani wanaposhinda wamekuwa wakipewa bonasi kati ya Sh150 milioni hadi 300 milioni.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwanaspoti umebaini kuwa Azam ndiyo timu inayofuatia kulipa bonasi vizuri kwani wanapokutana na Simba ama Yanga bonasi yake inakuwa kati ya Dola 10,000 sawa na Sh23 milioni hadi 20,000 zaidi ya Sh45 milioni.

Nyota wa Azam wanapocheza na timu nyingine nje ya Simba na Yanga imeelezwa kwamba bonasi zao zinakuwa chini ya Dola 10,000 napo inategemea na namna ambavyo mabosi wataamua. Hivyo bado Simba na Yanga wapo juu kwenye bonasi zao ukilinganisha na matajiri wa ligi hiyo, Azam FC.

“Katika mgawanyo wa bonasi hizo inategemea na timu na timu, kwani kuna baadhi bonasi inapotoka wanapewa wachezaji 18 yaani 11 wanaoanza na saba wanaokuwa benchi pamoja na benchi lao la ufundi ila wale ambao hawakucheza kabisa hawapati, lakini kuna timu nyingine zinatoa kwa wote yaani wale 18 na ambao wanakuwa jukwaani mfano ni majeruhi au hawakupata nafasi wanapewa pesa kidogo,” alisema kiongozi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

SOMA NA HII  VIGOGO WA SOKA AFRIKA...WAIOGOPA MECHI SIMBA NA YANGA...WAPATA VIGUGUMIZI

Ukiachana na timu hizo tatu vigogo, KMC inafuatia kwa kutoa bonasi kubwa kwa wachezaji wake kila wanaposhinda mechi za ligi kwani wamekuwa wakiwekewa Sh3 milioni mezani hivyo endapo fedha hizo zitagawanywa kwa wachezaji 18 waliohusika na mchezo wa siku hiyo pamoja na bechi la ufundi kila mmoja atavuna Sh150,000.

Timu nyingine inayotoa bonasi kubwa kwa wachezaji ni Mbeya Kwanza ambayo imepanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu huu.

Timu hiyo kila inaposhinda imekuwa ikitoa bonasi ya Sh3 hadi 5 milioni kulingana na mechi wakati Namungo wamekuwa wakitoa Sh2 hadi 3 milioni huku Kagera Sugar nao wakiwa si haba kwani wamekuwa wakitoa Sh2 milioni kila wanaposhinda mechi.

Mbeya City nao hawako nyuma kwa kutoa pesa ili kuwapa motisha wachezaji wao kwani kila timu hiyo inaposhinda mechi zake, kila mchezaji amekuwa wakivuna Sh100,000 hadi 150,000 kwa kila mechi wakati Polisi Tanzania kila mchezaji amekuwa akilamba Sh60,000 hadi 80,000 kila wanaposhinda mechi zao.

Biashara United wenyewe wamekuwa wakiwapa wachezaji wao Sh75,000 kila wanaposhinda mechi na Sh50,000 wanapotoka sare wakati kwa upande wa mechi za kimataifa wakishinda kila mchezaji hupata Sh100,000 huku Prisons kila mchezaji hupata Sh60,000 wakishinda huku Mtibwa Sugar ikitoa bonasi ya Sh50,000 kwa kila mchezaji kwa kila mechi wanayoshinda sawa wanavyofanya Dodoma Jiji.

Kwa upande wa Ruvu Shooting hutoa bonasi ya Sh1.2 Milioni kila mechi ambayo wanashinda huku Coastal Union ikitoa Sh1 milioni wakati Geita Gold yenyewe ilikuwa ikitoa Sh2 milioni kila mechi kwenye Ligi Daraja la Kwanza kabla haijapanda Ligi Kuu na kwa sasa bado haijajulikana kama itaongeza au bonasi hiyo itabaki hivyo hivyo kwa sasa.

Beki wa zamani wa Tanzania Prisons, Dickson Oswald alisema bonasi zinasaidia sana kuongeza ari ya upambanaji kwa wachezaji kwani mpira ni maisha.

“Mpira ni maisha ni kazi kama nyingine hivyo licha ya kwamba kushinda ni wajibu wa mchezaji lakini bonasi zinaongeza chachu fulani yakupambana uwanjani kwani mnakuwa mnajua kuwa tukifanya hivi pesa itaongezeka, alisema Oswald.

Naye kipa wa zamani wa Yanga, Simba, Azam na Ihefu, Deogratius Munishi ‘Dida’ alisema bonasi zinaongeza motisha kwa wachezaji na kuleta ari ya upambanaji uwanjani.

“Licha ya kwamba kucheza na kupata matokeo ni wajibu kwa mchezaji kwa sababu hiyo ndio kazi yetu lakini endapo mkiahidiwa bonasi kua mkishinda mtapata hiki, ile morali inakuwa kubwa zaidi na kuchangia ushindi,” alisema Dida.

Credit:- Mwanaspoti