Home Yanga SC HUYU HAPA MBADALA WA METACHA MNATA YANGA

HUYU HAPA MBADALA WA METACHA MNATA YANGA

RAZACK Siwa, Kocha wa Makipa wa Yanga amesema kuwa wanaweza kumtumia kipa namba tatu, Ramadhan Kabwili katika mechi zilizobaki ikiwa ni pamoja na ya leo dhidi ya Mwadui FC, Uwanja wa Mkapa.


Ikiwa mzawa Kabwili ataanza leo kukaa katika mlingoti wa lango la Yanga utakuwa mchezo wake wa kwanza ndani ya msimu wa 2020/21 ambapo Yanga imecheza jumla ya mechi 30  yeye hakuanza hata mchezo mmoja.

Pia Kabwili atakuwa ni mbadala wa kipa namba moja Metacha Mnata ambaye amesimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na suala la utovu wa nidhamu.

Siwa amesema kuwa kuna mechi ambazo zimebaki wanaamini wataweza kumtumia Kabwili ambaye hajapata nafasi ya kucheza.

Siwa amesema:-“Nafikiri mechi bado hazijaisha hivyo tumuombe Mungu nafikiri kwa mechi ambazo zimebakia tunaweza kumuona Ramadhan Kabwili akianza kwani huwa ninafundisha kila mchezaji kuweza kupata nafasi ya kucheza.

“Ninarudia kusema kuwa mapumziko tuliyopata wakati ule wa timu ya taifa yametufanya tuwe imara hivyo tunahitaji kupata matokeo chanya katika mchezo wetu dhidi ya Mwadui FC,” amesema Siwa.

Nahodha Msaidizi Ramadhan Kabwili amesema kuwa anaamini kuwa mechi sio kazi ngumu kuliko mazoezi hivyo yupo tayari kucheza. 

“Ninaamini kwamba mazoezi ni magumu kuliko mechi hivyo kwangu mimi nipo tayari tusubiri tuone kocha atampanga nani kama ataanza Shikalo, (Farouk), kama ni Metacha, (Mnata) sawa sisi wote ni timu moja tunahitaji ushindi,”  amesema Kabwili.

Frederick Masombola, Kocha Msaidizi wa Mwadui FC, amesema kuwa kupoteza mechi mbili mbele na Yanga kumewaongezea umakini hivyo watapambana kupata ushindi.

“Tumecheza mechi mbili na Yanga ile ya mabao 5-0,(ligi) na ule wa pili tulifungwa mabao 2-0,( FA) hivyo tumejipanga na wachezaji wapo tayari kisaikolojia ukizingatia kwamba wapo wengine ambao tuliwasajili dirisha dogo hawakuwepo mechi ya kwanza,” amesema.

Mussa Mbissa nahodha wa Mwadui FC amesema kuwa wachezaji wamekubaliana kutafuta ushindi Kwenye mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA YANGA KITAKACHOANZA LEO DHIDI YA ALTABARA KAGAME CUP