Home Ligi Kuu LALA SALAMA KILA TIMU IPAMBANE, MABORESHO YA VIWANJA NI MUHIMU

LALA SALAMA KILA TIMU IPAMBANE, MABORESHO YA VIWANJA NI MUHIMU


 IKIWA ni lala salama hapo kwenye Ligi Kuu Bara kuna mambo ambayo ni muhimu kuanza kutazamwa kwa sasa hasa kwa upande wa ushindani pamoja na usajili wa wakati ujao.

Kimbembe kinaanza kwa wachezaji wenyewe ambapo kwa sasa unaona kwamba wanacheza kwa kujitoa kwa ajili ya kutafuta matokeo ndani ya uwanja.

Ukiwaweka kando hao wachezaji pia benchi la ufundi, viongozi nao wamekuwa bega kwa bega kutoa sapoti wakishirikiana kwenye kutimiza majukumu yao uwanjani.

Hali hii inaleta picha nzuri kule ambako tunatarajia kwenda kutokana na kila mmoja kuwa na kitu ambacho anakifikiria kwa sasa na anakitenda kwa wakati.

Wale ambao wapo Ligi Daraja la Kwanza wanajua kile ambacho wamekivuna kwani tayari Geita na Mbeya Kwanza wameshapanda na zile za kushuka ikiwa ni Njombe Mji, Mbao, Lipuli zimejua fungu lao wakati ujao.

Hamna namna ya kufanya kwa sasa kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kwa kuwa kwenye ushindani ni lazima aonekane ambaye anashindwa. Lazima itatokea wapatikane wa kushuka na wale wa kupanda.

Njombe Mji wanaanza maisha Ligi Daraja la Pili, wana kazi ya kufanya ili kuweza kupeperusha bendera ya mashabiki wake wakizubaa wataangukia pua wakati ujao.


Kushindwa kwa sasa haina maana kwamba wao sio bora hapana ni hesabu tu zimewagomea  wanaweza kujipanga upya wakarudi wakaendelea na kasi yao ile walipokuwa wanaanza msimu.

Ndugu zetu Mwadui FC wana uhakika wa kushiriki Ligi Daraja la Kwanza ni muda wao kuanza kujipanga kwa wakati ujao licha ya kuwa wana mechi za kukamilisha ratiba kwenye ligi.

Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.

Ila imekuwa bahati mbaya kila wakati timu nyingi kuanza kuonyesha ushindani kwenye mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama jambo ambalo linawaongezea ugumu kufanya vizuri.

Zile ambazo zinapanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza zina kazi kubwa ya kuanza kufanya maandalizi ili ziweze kuleta ushindani wa kweli ndani ya ligi.

Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.

Stand United ilikuja ikashuka na ikashuka tena pale ilipokuwa kwenye Ligi Daraja la Kwanza. Singinda United ilikuja kwa kasi ila ghafla nayo kasi imekata na sasa hata Ligi Daraja la Kwanza nako imeshushwa.

SOMA NA HII  KMC YATIA TIMU RUKWA, KAMILI KUIVAA TANZANIA PRISONS

 Matukio haya yawe darasa kwa timu ambazo zinapambana kupanda kwenye ligi nazo zinapaswa zijue kwamba huku juu mambo sio mepesi kama ambavyo wanafikiria.

Matumaini yangu ni kwamba kupitia matukio haya yanayoendelea wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.

Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.

Ukiachana na ligi kuu ya wanaume pia kuna ligi ya wanawake hapa pia kuna umuhimu wa kuitazama kwa ukaribu ili kutengeneza timu makini pia kwa wanawake.

Kutokana na ushindani uliopo hasa kwenye timu za wanawake kuna umuhimu wa wadau kujitokeza pia kutoa sapoti kwa wanawake ili nao pia waweze kuleta ushindani.

Bingwa wao nao ameshapatikana hivyo wanapaswa wapewe pongezi ambao ni Simba Queens kwa zile nyingine ambazo zimekwama zina muda wa kujipanga kwa wakati ujao.

Zawadi kubwa huku iwe kwenye kuwaboreshea mazingira yao ya kazi hasa kuanzia viwanja pamoja na vitendea kazi.

Katika hili pia iwe fundisho katika kuangalia usalama na uwepo wa wachezaji wetu kwani wanajitoa kwa ajili ya kazi kwa kufanya mchana hata usiku ila hakuna ambaye anawajali.

Kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama namna ya kuwapiga tafu wachezaji pamoja na timu kiujumla kwani wengi hali zao bado hazijawa sawa.

Mazingira magumu ya maandalizi yanafanya timu iweze kufungwa mabao mengi kwenye mchezo mmoja hili jambo sio nzuri kwani tunahitaji kuona ushindani wa kweli.

Katika hili ni muhimu kutazama namna maandalizi yalivyo pamoja na fedha ambazo zinatumika kwenye maandalizi kamili kwa timu.

Timu chache zina uhakika kuhusu posho na stahiki za wachezaji na hii ni mbaya kwani mambo yakiwa hivi ushindani utazidi kupungua.

Wakati mwingine tunashindwa kuwa na timu bora inayoshiriki kwenye ligi ya wanawake ambayo itasaidia kupata na kuibua vipaji.

Kwa namna mambo yanavyokwenda hii haileleti afya katika maisha ya soka na ili uweze kuushinda mpira na kupata matokeo ndani ya uwanja ni lazima kupambana.

Pia kuna suala la usajili ni muhimu kwa timu zote kuangalia kwa umakini namna inavyowezekana kwa ajili ya kujenga timu.