Home Ligi Kuu RUVU SHOOTING: HASIRA ZA SIMBA, TUNAWAMALIZIA YANGA

RUVU SHOOTING: HASIRA ZA SIMBA, TUNAWAMALIZIA YANGA

 


BAADA ya kipigo cha mabao 3-0 walichokipata kutoka kwa Simba Alhamisi iliyopita, Uongozi wa kikosi cha klabu ya Ruvu Shooting umetamba kuwa, sasa hasira zao zote wanazihamishia kwenye maandalizi ya mchezo wao ujao dhidi ya Yanga utakaopigwa Juni 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa.

Kipigo dhidi ya Simba, ni cha nne mfululizo kwa Ruvu Shooting na kinaifanya klabu hiyo izidi kuporomoka kutoka nafasi ya nne ambayo walikuwepo mwanzoni mwa msimu huu, mpaka nafasi ya kumi ya msimamo baada ya kujikusanyia pointi 37 katika michezo 30 waliyocheza mpaka sasa.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza timu hizo zilipokutana Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 mchezo uliopigwa Desemba 6, mwaka jana kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Mchezo wa Juni 17, pia utapigwa katika uwanja wa Mkapa.

Akizungumzia mpiango yao, Ofisa habari wa klabu ya Ruvu, Masau Bwire amesema: “Tumesikitishwa na matokeo ya mchezo wetu uliopita dhidi ya Simba, kwa bahati mbaya kipigo hicho kimetufanya tupoteze mchezo wa nne mfululizo, hii ni baada ya kupoteza mbele ya Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Mbeya City.

“Kutokana na matokeo hayo tumeshuka kutoka nafasi ya nne tuliyokuwepo hapo awali, mpaka nafasi ya kumi, kama uongozi hatujafurahishwa na hali hii na sasa tumejipanga vizuri kumaliza makosa tuliyoyaonyesha, na tutahakikisha tunaanza mapema maandalizi ya mchezo wetu ujao dhidi ya Yanga ambao ni lazima tuhakikishe tunapata pointi tatu muhimu katika mchezo huo.”

SOMA NA HII  MSIMAMO WA LIGI KUU TANZANIA BARA