Home Tetesi za usajili WINGA DODOMA JIJI NI SUALA LA MUDA TU KUTUA YANGA

WINGA DODOMA JIJI NI SUALA LA MUDA TU KUTUA YANGA

 


ALLY Mohamed ambaye ni meneja wa winga wa Dodoma Jiji FC, Dickson Ambundo, amefunguka kuwa mteja wake huyo atakuwa mchezaji rasmi wa Yanga siku za hivi karibuni kwa kuwa kila kitu kinaelekea kukamilika.

 

Meneja huyo alisema walishapokea ofa kutoka Yanga na wameshafikia kwenye asilimia zaidi ya 90 ili mchezaji huyo kusaini dili hilo, hivyo hakuna namna ambayo inaweza kushindikana.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Ally alisema: “Yanga tumeshafika nao katika hatua nzuri ya kukamilisha hili dili, kwa sababu waliwasilisha ofa na tukawa tumefikia kwenye hatua nzuri sana na ndiyo maana naweza kusema mambo yapo vizuri kabisa na hakuna shida.”Spoti Xtra lilimtafuta Ambundo ili kujua kuhusu yeye, ambapo alisema:

 

“Kiukweli kila kitu nimemuachia meneja na uongozi wangu uweze kusimamia kila kitu, kazi yangu mimi ni kucheza soka na siyo kitu kingine.”

 

Taarifa kutoka Kambi ya Dodoma Jiji zimeeleza kuwa, Ambundo amegoma kuongeza mkataba na ameshawaaga wenzake kuwa anatimkia zake Yanga msimu ujao.


Ambundo msimu huu Dodoma Jiji ikiwa imetupia jumla ya mabao 28 amefunga matano na kutoa pasi nne za mabao.

Leo Juni 23 timu yake itakuwa na kazi ya kufanya mbele ya Gwambina FC kwenye mchezo wa ligi utakaochezwa Uwanja wa Gwambina Complex.

SOMA NA HII  BAADA YA KUMWEKA SOKONI MUKOKO...UONGOZI YANGA WAFUNGUKA HAYA KUHUSU DIARA..