BENCHI la Ufundi la Yanga lililo chini ya Kocha Mkuu raia wa Tunisia Nasreddine Nabi wametumia siku mbili sawa na saa 48 kuangalia video tatu za mechi za mwisho za watani wao Simba kabla ya kuvaana nao.
Hiyo ni katika kuelekea Kariakoo Dabi itakayopigwa leo Jumamosi saa kumi na moja kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Nabi jana Alhamisi na leo Ijumaa saa mbili usiku alitarajiwa kufanya kikao na wachezaji wake sambamba na kuangalia video tatu za mechi za mwisho ambazo wamezicheza wapinzani Simba.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kati ya mechi hizo ipo ya Nusu Fainali ya Kombe la FA waliyocheza dhidi ya Azam FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Songea iliyoamalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone.
Aliongeza kuwa benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo walitumia muda huo kuangalia video hizo za mechi kwa lengo la kuangalia upungufu na wachezaji hatari watakaokwenda kuwachunga kwa lengo ya kuwazuia.
“Kocha Nabi amekuwa na ratiba ya kuangalia mchezo mmoja wa wapinzani kabla ya kwenda kukutana nao, lakini katika kuelekea mchezo huu ameongeza video tatu tofauti na awali.
“Hiyo ni katika kuhakikisha anawasoma vizuri wachezaji wa timu pinzani ili kuhakikisha anafanikisha malengo yake ya ushindi kwenye mechi hiyo.“
Hivyo atatumia michezo hiyo mitatu kujua mbinu na wachezaji hatari atakaokwenda kukutana nao, tayari kocha amefanya maandalizi ya kikosi chake katika kuelekea mchezo huo muhimu wa ligi ili kuhakikisha anazuia ubingwa wa ligi,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafuta Mwenyekiti wa Kamati wa Ufundi wa Yanga, Dominic Albinus kuzungumzia hilo simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.Aidha Championi Ijumaa lilimtafuta Meneja wa timu hiyo, Hifidh Saleh kuzungumzia hilo alisema: “Hilo suala atafutwe Ofisa Habari, Hassani Bumbuli ndiye anayezungumzia masuala ya timu.”