KUELEKEA mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, kocha mkuu wa kikosi cha Azam, George Lwandamina amefunguka kuwa wanataka kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo, ili kuvuna ushindi wa pointi tatu muhimu zitakazowaweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo.
Azam watakuwa wenyeji wa Simba Julai 14, mwaka huu katika mchezo huo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Timu hizo zitaingia katika mchezo huu zikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Februari 7, mwaka huu.
Akizungumzia maandalizi yao, kocha Lwandamina amesema: “Hatukuwa na matokeo mazuri sana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Namungo, na tuna mchezo mgumu mbele yetu dhidi ya Simba, lakini sina shaka kwa kuwa tumekiandaa kikosi chetu kushindana na kushinda mchezo huo, na kujiimarisha zaidi kwenye msimamo.”
Naye Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ kuhusu maandalizi hayo amesema: “Tumeanza mapema maandalizi yetu dhidi ya Simba kwa kuwa tunatambua umuhimu na ugumu wa mchezo huu, tutacheza na timu bora lakini kama wenyeji wa mchezo huo tuna kila sababu ya kuibuka na ushindi.”