JEMBE jipya la Yanga, Mkongomani Djuma Shabani amefunguka kuwa anavutiwa na uwezo wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Yacouba Songne na anaamini uwezo wake utaisaidia Yanga kufikia malengo yao msimu ujao.
Beki huyo wa kulia amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga ambapo alikuwa na kiwango bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na kikosi cha AS Vita, akifunga mabao mawili na asisti tatu, huku akitupia mabao matano na asisti sita kwenye Ligi Kuu ya DR Congo.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Djuma alifunguka kuwa: “Kikosi cha Yanga kina wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kuipa mafanikio makubwa, nimekuwa nikiwafuatilia kwa ukaribu kwenye mechi za hivi karibuni.
“Wapo wachezaji ambao navutiwa na aina yao ya uchezaji, kwa mfano Yacouba Songne ni moja ya wachezaji wa Yanga ambao ninavutiwa na aina yake ya uchezaji.
“Pia wachezaji kama Kisinda na Mukoko ni miongoni mwa wachezaji ambao pia navutiwa na aina yao ya uchezaji wao, hivyo ninaamini kwa umoja wetu tutapambana kuisaidia timu kufikia malengo yake kwa msimu ujao ambayo ni kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na kutwaa ubingwa.”