HATIMAYE taji la Euro 2020 linakwenda Roma baada ya mpango wa kuelekea England kubuma katika mchezo wa fainali iliyopigwa usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Wembley.
Mbele ya mashabiki 67,173 ubao ulisoma Italia 1-1 England na vijana wa Gareth Southgate walishindwa kutwaa taji hilo kwa kufungwa penalti 3-2. Walianza England kufunga bao la mapema lilifungwa na Luke Shaw dk 2 lilisawazishwa na Leonardo Bonucci dk 67.
Nyota watatu wa England walishindwa kufunga penalti ambao ni Marcus Rashford tuta lake liligonga mwamba, Jadon Sancho pamoja na Bukayo Saka ni mikono ya Gianluigi Donnaruma kipa wa Italia iliokoa jambo lililofanya mpango wa kupeleka taji la Euro England kuwa gumu kufanikiwa.
Matumaini ya kubeba taji la kwanza kwa England baada ya miaka 55 yalianza kupatikana katika changamoto za penalti baada ya Jordan Pickford kipa wa England kuoka penalti ya Andrea Belotti mwisho wa siku ndoto yao ya muda mrefu ikayeyuka mazima.
Southgate, Kocha Mkuu wa England amesema kuwa aliwachagua vijana wa kupiga penalti kulingana na mazoezi ambayo walifanya hivyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ni juu yao wenyewe kwa kuwa walikuwa wanahitaji kutwaa taji hilo.
“Ilikuwa ni jukumu la kila mchezaji kutimiza kazi yake, kwa upande wa penalti wale ambao walifanya mazoezi niliwapa jukumu hilo. Lakini imekuwa ngumu kwetu kufanikiwa kwa kuwa kipindi cha pili wachezaji wanajua wenyewe ambacho walikuwa wanakifanya,” .
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Italia, Roberto Mancini amesema kuwa ilikuwa ni jambo lisilowezekana kutabiri ushindi mapema, huku akitoa pole kwa England.
“Ilikuwa ni ngumu kutabiri nani atatwaa taji hasa ukizingatia kwamba England nao walikuwa wanalihitaji. Kushinda kwa penalti unaweza kusema ni bahati lakini vijana wanahitaji pengezi. Pole kwa England kwa hili ambalo limetokea,”.