TANGU Jumapili iliyopita stori kubwa kwenye mitandao ya kijamii hasa ile ambayo tunaifuatilia sisi wapenzi wa mchezo wa soka hapa nchini, ishu kubwa imekuwa ni suala la ujio wa basi jipya la klabu ya soka la Yanga.
Basi hilo tayari limewasili Tanzania na kuna uwezekano mkubwa kwa sasa likawa gereji kwa ajili ya kulifanyia maandalizi ya mwisho, ikiwemo kuliwekea stika za matangazo ya wadhamini wa klabu hiyo tayari kwa ajili ya kuanza kutumika na wachezaji wa klabu hiyo.
Basi hilo aina ya Scania Irizar limetolewa na mdhamini wa klabu hiyo mfanyabiashara, Ghalib Said Mohammed anayejulikana zaidi kwa ufupisho wa jina lake ambao ni GSM.
Ndinga hilo linatajwa kumgharimu bosi huyo kiasi cha zaidi ya Shilingi Milioni 900 za kitanzania, huku hesabu yake mpaka itakapotoka gereji ikitajwa kufikia Shilingi Bilioni moja na ‘chenjichenji’.
Kwanza kabisa naupongeza uongozi wa Yanga pamoja na mdhamini wao GSM, kwa kuendelea kufanya mapinduzi mbalimbali ya kiudhamini wa klabu hiyo ambao unazidi kuongeza thamani ya kikosi hicho.
Huu ni mwendelezo wa mambo mengi mazuri na yenye manufaa makubwa kwa soka la Tanzania, yanayoendelea kufanywa na Yanga chini ya udhamini wa GSM. Chini ya mfanyabiashara huyo tumeishuhudia Yanga ikifanya maboresho makubwa ya kikosi chao kwa usajili wa wachezaji wengi bora mwanzoni mwa msimu uliopita.
Lakini GSM pia ndiyo ambao wamejitolea kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha wanakamilisha mchakato wa mabadiliko ya kiundeshaji wa klabu hiyo kwa kutoa fungu la fedha za kuwezesha mchakato huo, kuanzia hatua za awali mpaka ulipokamilika, na kupitishwa kwenye mkutano mkuu wa Wanachama wa Yanga uliofanyika Juni 27 mwaka huu.
Lakini pia ni chini ya uongozi huo tumeona Yanga ikifanikiwa kusaini makubaliano ya kimkataba wa haki za matangazo ya Televisheni na kampuni ya Azam Media, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 34.8 za Kitanzania.
Kwa watoto wa mtaani hii tunaiita gari limewaka, bila shaka kuna mengi yanatarajiwa zaidi, kwa ajili ya furaha ya mashabiki wa klabu hiyo kongwe ambao kwa sasa hawashikiki kwa ‘kujimwambafai’ huku mitaani.
Mashabiki wa Yanga kwa sasa wanaonekana kuzidiwa na furaha ya vifurushi vya zawadi za furaha wanavyopokea, walianza na ushindi dhidi ya Mtani wao Simba, wakapata mabilioni ya Azam, na sasa basi jipya.
Kutokana na kelele za Yanga na basi lao jipya, mashabiki wa Simba nao wamekuwa wakiwajibu kiutani Yanga kuwa, wasijisahaulishe na basi jipya wakati Injinia aliwaahidi ubingwa.
Kwangu nadhani kuna pointi kubwa ambayo inatoka kwenye utani huu, kwani mwanzoni mwa msimu huu kulikuwa na kauli mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa Yanga kuhusiana na malengo yao ya kushinda kombe la Ligi Kuu Bara.
Mfano ni pale Ofisa mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz aliyeahidi Yanga wangetwaa ubingwa kabla ya michezo yao 10 ya mwisho.
Labda zilikuwa tambo tu, lakini tukirejea kwenye uhalisia ni wazi ubingwa wa Ligi Kuu ni miongoni mwa mahitaji makubwa ya Yanga kwa misimu minne mfululizo sasa.
Jambo la kujiuliza zaidi kao ni kwamba, katika kipindi chote hiko ni Mtani wao Simba ndiye amekuwa mtawala wa kombe hilo.
Heshima ya klabu yoyote duniani, ni ubora walionao katika kutawala soka la nchi ambayo klabu hiyo inatoka (kwa kutwaa makombe), na tunaona hili kwa klabu kama Bayern Munich ya Ujerumani, Al Ahly ya Misri na nyinginezo.
Hii pia hutoa faida ya bingwa kuwa mwakilishi wa nchi katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, hivyo ishi ya Simba kutangaza ubingwa kwa misimu minne mfululizo si jambo la kuchukuliwa poa kabisa na wadau wa Yanga.
Kuna msemo usemao ‘acha mvua inyeshe tuone panapovuja’, hii ina maana kwamba hii mvua ya utawala wa makombe ya Ligi Kuu huko Simba, inadhihirisha kuna mahali pale Yanga kunavuja.
Katika hili uongozi wa kikosi cha Yanga unapaswa kukaa chini na kuangalia ni wapi wanakosea hatua, kiasi cha Mtani wao kujimilikisha makombe kila kukicha.
Ifike wakati waambizane ukweli na kuacha kufichana, ni kweli basi jipya ni muhimu sana Yanga, lakini lisitumike kuwasahaulisha mashabiki wa Yanga juu ya ahadi ya ubingwa mliowapatia.
Injinia Hersi, naomba unisaidie kumwambia bosi Ghalib Yanga wanahitaji ubingwa kuliko wanavyolihitaji basi jipya.