MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Argentina na klabu ya Barcelona, Leonel Messi anatarajiwa kuisaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Barcelona kwa miaka mitano zaidi.
Messi amekubali kusaini mkataba huo licha ya kwamba utahusisha makato ya mshahara wake kwa asilimia 50 kutokana na miongozo ya La Liga. Mkataba huo utamfanya Messi aendelee kusalia ndani ya Barcelona mpaka atakapokuwa na umri wa miaka thelathini na tisa.
Mkataba uliopita wa Messi ndani ya Barcelona ulikuwa ukimfanya nyota huyo kuvuna kiasi cha Euro Milioni 425 kwa kipindi chote cha miaka minne ambacho kilimalizika Juni 30, mwaka huu.
Rais wa Barcelona amekuwa akifanya kila jitihada za kuhakikisha staa huyo anaendelea kusalia ndani ya kikosi cha Barcelona baada ya dirisha hili la usajili la majira ya Kiangazi.
Katika kipindi ambacho Messi amekuwa mchezaji huru baadhi ya klabu kama Manchester City na Paris St German zilionyesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 amekuwa kwenye kituo cha kukuzia vipaji cha Barcelona tangu mwaka 2000, ambapo ameichezea Barcelona michezo 778 na kufunga mabao 672.