BAADA ya kusambaa sauti kwenye mitandao ya kijamii ikimhusisha Msemaji wa Simba, Haji Manara akimtuhumu Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez hatimaye amefunguka jambo juu ya hilo.
Sauti hiyo ilianza kusambaa muda mfupi baada ya Manara kuandika kwenye akaunti yake ya Instagram akidai kufanyiwa visa na mambo mabaya na kusingiziwa, akimtuhumu Barbara.
Manara alienda mbali zaidi na kudai anashutumiwa kuihujumu timu hiyo akidaiwa kukutana na viongozi wa Yanga maeneo ya Kariakoo na Kigamboni.
“Mimi sinunuliki kwa thamani yeyote ya pesa, unataka kunifedhehesha mimi, watu gani mimi hata gari yangu ilipita Posta, Kigamboni mimi naendaje, kwahiyo mimi nitoke Posta niende Kigamboni kwenye kambi ya wale,” amedai Manara
Baada ya kuongea kwa jazba Manara alishuka na kusema anasubiri mechi ya Jumapili Julai 25 dhidi ya Yanga kuisha atazungumza zaidi.
Hata hivyo, Barbara alipoulizwa mapema leo asubuhi amesema amesikia maneno hayo, lakini kwa sasa akili zake zipo kwenye mechi yao ya Fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya watani wao, Yanga kisha mengine yatafuata.
“Nimesikia hayo maneno, focus yangu kushinda mechi ya Jumapili, mengine yatafuata,” amesema Barbara kwa ufupi.
Simba na Yanga zitakutana kwenye mchezo huo wa fainali itakayochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma, huku ikiwa ni wiki chache tangu zilipovaana katika mechi ya Ligi Kuu Bara jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ya Julai 3, Yanga ilishinda bao 1-0 lililowekwa kimiani na Zawadi Mauya.
Hata hivyo, katika msimu uliopita wa ASFC, Simba na Yanga zilikutana kwenye mechi ya nusu fainali na Yanga kucharazwa mabao 4-1.